Imam wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ismaili na Mwenyekiti wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Aga Khan, anatarajia kuwasili nchini kesho kwa ziara ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais John Magufuli.
Mratibu wa Mawasiliano wa Jumuiya ya Aga khan, Aly Ramji, amesema ziara hiyo imelenga kupanga mikakati zaidi ya kukuza ushirikiano kati ya Mtandao wa AKDN na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi wake.
“Ujio huu wa Aga khan nchini Tanzania ni muhimu sana kwani mbali na kualikwa na rais, lakini pia wataweza kujadili mambo mbalimbali katika hatua ya kukuza ushirikiano na kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali.
“Taasisi za AKDN ni kati ya mashirika makubwa ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania na huchangia maisha ya Watanzania wote, hivyo naamini kupitia ujio huu, utazaa matunda zaidi,” amesema Ramji.
Aidha, amesema Aga Khan atapokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga.
No comments:
Post a Comment