Saturday, September 30

Waliopata sifa ujenzi wa maabara, madawati kumbe walikiuka taratibu


Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa barabara Joseph
Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa barabara Joseph Haule 

Dodoma. Bodi ya Mfuko wa Barabara imesema baadhi ya halmashauri zilizosifiwa katika ujenzi wa maabara na ununuzi wa madawati, zilitumia fedha za ujenzi wa barabara kinyume cha utaratibu.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Joseph Haule alisema jana mjini hapa kuwa, katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2015 wamebaini kuwa halmashauri saba zimetumia Sh359.5 milioni zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwenye ujenzi wa maabara na ununuzi wa madawati.
Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Karagwe ambayo ilitumia Sh55.5 milioni, Masasi (Sh31.2 milioni), Nanyumbu (Sh110.6 milioni), Kilolo (Sh102.3 milioni), Songea (Sh7.3 milioni), Kyerwa (Sh36.8 milioni) na Ushetu (Sh15.7 milioni).
“Tena wakapongezwa, kumbe wametumia mbinu ovu za kutimiza lengo lile wameihadaa Serikali walitakiwa watumie vyanzo vyao vya mapato, hizi fedha kwa mujibu wa sheria zimepangwa na kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa barabara,” alisema.
Alisema, “Bodi ya Mfuko wa Barabara inasema warudishe fedha zile kutokana na vyanzo vyao zikafanye shughuli iliyokusudiwa na iliyokuwa approved (idhinishwa) na Bunge.”
Bodi pia imeazimia kupeleka taarifa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kuwachukulia hatua stahiki watumishi waliohusika na ubadhirifu wa fedha za mfuko huo na kuisababishia Serikali hasara.
Maazimio ambayo tayari yamo katika ripoti ya bodi hiyo ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja katika mamlaka za halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji Tanzania Bara katika mwaka wa fedha 2014/15 na 2015/16.
Haule alisema miongoni mwa ubadhirifu huo ni malipo hewa kwa kazi zisizofanyika, kukosekana kwa nyaraka za malipo, matumizi ya fedha za mfuko wa barabara yasiyofuata kanuni na mikataba wakati wa utekelezaji na miradi kujengwa chini ya viwango.
Halmashauri zilizobainika kuwa na dosari katika ukaguzi huo ni Gairo, Kalambo, Kakonko, Kondoa, Meru na Ngorongoro.
Malipo hewa
Mbali ya ubadhirifu huo. Haule alisema katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 2015, CAG pia alibaini kuwa halmashauri nne nchini zililipa malipo kwa kazi zisizofanyika zenye thamani ya Sh77.4 milioni.
Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni ya Moshi (Sh12.7 milioni), Monduli (Sh6.6 milioni), Mtwara (Sh46 milioni) na Tanga (Sh12.1 milioni).
Haule alisema bodi hiyo imeazimia kuwa wahandisi waliohusika na miradi ambayo haikujengwa kwa kuzingatia viwango wasihamishiwe katika Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) na wahandisi wasiosajiliwa wasipewe kazi katika wakala huo.
“Bodi inamuomba katibu mkuu Tamisemi kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale wote waliohusika kuisababishia Serikali hasara na kuchelewesha utekelezaji wa miradi,” alisema.

No comments:

Post a Comment