Dar es Salaam. Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatarajia kuzindua jukwaa la kitaifa la wadau wa sekta mtambuka katika usimamizi wa rasilimali za maji.
Jukwaa hilo litazinduliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge Jumatano Oktoba 4 jijini hapa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo katika taarifa amesema uzinduzi huo umeandaliwa na wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya 2030 Water Resources Group.
Amesema baada ya uzinduzi kitafanyika kikao cha kwanza cha jukwaa Oktoba 5 ambacho kitajadili changamoto za usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.
Dk Mkumbo amesema kuzinduliwa kwa jukwaa hilo ni fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau kutoka sehemu mbalimbali za dunia na hasa kuhusu utekelezaji wa mipango ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Amesema jukwaa linatarajiwa kutoa ushauri kwa wizara kuhusu namna bora ya kuboresha ushirikiano baina ya sekta mbalimbali katika usimamizi wa rasilimali za maji, hivyo kurahisisha uamuzi wa Bodi ya Maji ya Taifa na Bodi za Maji za Mabonde.
Jukwaa hilo pia litatoa mchango wa mambo ya kupewa kipaumbele na Kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji kinachotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.
“Jukwaa litahusisha wadau na washirika mbalimbali wa maji kujadili, kuchangia mawazo na kubuni njia zitakazowezesha upatikanaji na usalama wa maji,” amesema.
Amesema jukwaa litawezesha wadau kujifunza, kutoa maoni, ujuzi na kushauri kuhusu masuala ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.
Chimbuko la kuanzishwa jukwaa hilo ni kutokana na changamoto zinazotokana na uratibu hafifu wa sekta, taasisi na wadau katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.
Changamoto hizo zimesababisha kupungua na kukauka kwa vyanzo vya maji na kuongezeka kwa migogoro kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji kwa shughuli za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment