Inasikitisha sana kuona madini ambayo yako Tanzania tu, lakini nchi ya India ndiyo inaonekana ni ya kwanza duniani kuyazalisha. Tumesikia jinsi maelfu ya watu huko India, wanavyopata ajira kutokana na viwanda vya Tanzanite nchini humo. Ni wazi Tanzanite imewanufaisha zaidi watu wa nje kuliko wa ndani.
Hivyo juhudi zozote za kudhibiti wizi huu mkubwa ni za kupongezwa sana. Pamoja na pongezi hizi, tunafikiri uamuzi huu wa kujenga ukuta umechelewa sana, maana taarifa zilizopo ni kwamba Mererani inakaribia kuwa mashimo matupu. Lakini pia kujenga ukuta wa kuzuia wizi wa madini kabla ya kujenga kiwanda cha kuongeza thamani ya madini haya, tatizo litabaki palepale.
Tanzanite zitatoka kwenye ukuta na kuelekea India ili kuongezewa thamani. Wale wanaoajiriwa kwenye viwanda vya India wataendelea kunufaika. Nini kianze, swali lilelile la yai na kuku. Labda kiwanda cha kuongeza thamani Tanzanite, Kingeanza kabla ya ukuta.
Lakini pia tunafikiri kitu muhimu ni kujenga ukuta kwenye vichwa vyetu. Ukuta unahitajika kwenye akili zetu na roho zetu. Bila kujenga ukuta kwenye akili zetu, ni kazi bure.
Si kwamba ninapinga ujenzi wa ukuta ambao Jeshi letu la ulizi limeanza kujenga kule Mererani, lakini tukiangalia mifano ya matukio katika Taifa letu ni kwamba bila kujenga ukuta vichwani mwetu, ni kazi bure.
Tuna mfano mzuri wa Mwadui. Hakuna mgodi, Afrika Mashariki wenye ukuta kama mgodi kama ule wa Mwadui. Pamoja na kuwa na ukuta huo wa Mwaduni, tumeibiwa zaidi ya miaka 50 na juzi tu almasi za mabilioni zimekamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina kuta imara kabisa, lakini tumeshuhudia jinsi wizi mkubwa umekuwa ukitokea kwenye BoT. Ufisadi mkubwa kwenye Taifa letu unaendelea kwenye taasisi zenye kuta kubwa na imara.
Hivyo tatizo si kujenga ukuta wa saruji na matofali, bali ni kujenga ukuta wa kumkomboa Mtanzania kifikra.
Mtanzania ajitambue, ajipende na kulipenda Taifa lake. Tunaweza kujidanganya, kama ambavyo tumekuwa tukijidanganya kwamba kazi hii ya kumkomboa Mtanzania kifikra itafanywa na wanasiasa wetu. Tunawaamini, tunawachangua, lakini wakifika kule, wanatugeuka.
Badala ya kuangalia masilahi ya Taifa, wanayashughulikia matumbo yao. Tuliwaamini watutengenezee Katiba mpya, lakini hadi leo hatujitambui na Katiba mpya imepaa na kupotelea kusikojulikana. Tuliwaamini watuletee maendeleo, lakini kila siku tunashuhudia meli zinaelea juu ya bahari lakini shilingi inazama. Tuliwaamini watuwakilishe bungeni, lakini kila kukicha tunashuhudia wanatetea masilahi ya vyama vyao vya siasa na kutuacha njia panda.
Njia pekee ya kupambana na wizi, ufisadi na udanganyifu katika Taifa letu na majanga mengine kama umaskini na ujinga, vita na upweke, ni kujenga mifumo ya watu kuishi kwa uwazi na kujaliana.
Ni lazima tujenge mifumo itakayotengeneza jumuiya za Watanzania zinazojaliana, zinazojuliana hali, zinazochungana, zinazolindana na zinazowajibishana.
Jumuiya za Watanzania tulizonazo sasa hivi, familia za Watanzania tulizonazo sasa hivi, ambazo zinashuhudia wizi mkubwa wa rasilimali za taifa letu na zinaishi kwenye upepo mkubwa wa ufisadi na wizi mkubwa ni zile ambazo kila mtu yuko kivyake.
Hakuna anayemchunga mwenzake, hakuna anayemlinda mwenzake na hakuna anayemwajibisha mwenzake. Kila mtu amejifungia katika nafsi yake: Hakuna uwazi katika familia, hakuna kufunuliana familia, hakuna kushirikishana katika familia, hakuna kuchukuliana familia, hakuna kulindana na kuchungana katika familia.
Hivyo hivyo hakuna uwazi katika jumuiya zetu, hakuna kufunuliana katika jumuiya zetu, hakuna kushirikishana katika jumuiya zetu, hakuna kuchukuliana katika jumuiya zetu, hakuna kulindana na kuchungana katika jumuiya zetu.
Kila mtu anaufunga moyo wake na kubaki na siri nyingi ndani ya nafsi yake. Hata na mambo ya kawaida kama vile kupenda, yanafanywa siri. Mambo kama tamaa, uchu, furaha, huzuni na mengineyo yanabaki siri ndani ya moyo wa mtu.
Kuna waandishi wengi, mfano kama Elieshi Lema wameandika juu ya tabia hii ya mtu kujifunga ndani ya nafsi yake. Ukipata nafasi unaweza kujisomea vitabu kikiwamo cha “Parched Earth”.
Mtu anayeufunga moyo wake hawezi kufanikiwa kutengeneza familia yenye kutoa mchango wa kulijenga taifa.
Ni lazima tuwe na mfumo imara na wa kudumu kuyakabili majanga yanayoweza kutukumba kimwili na kiroho. Mfumo wa sasa hivi ni ule unaotukuza wizi. Mtu akiiba ndiye mwanaume. Ukifanya kazi bila kuiba, bila kujenga nyumba kubwa ambayo haiendani na mshahara wako, unaitwa rofa. Katika jamii ambayo inautukuza wizi, kujenga ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite ni kupoteza nguvu na fedha.
Ngugi wa Thiong’o, katika kitabu chake cha Shetani Msalabani, anaelezea vizuri jinsi Waafrika tunavyowatukuza wezi. Anaelezea vizuri majigambo ya wezi, kuanzia wizi wa kuiba kuku na kuchomoa kwenye mifuko ya watu hadi wezi wakubwa wanaopora mali ya umma. Hatimaye heshima na umaarufu wa mtu katika jamii, unajengwa na kiwango kikubwa cha wizi. Ngugi, anaelezea vizuri kwenye kitabu hicho jinsi ilivyo kazi ngumu kuleta mabadiliko kwenye jamii yenye ugonjwa wa kuwatukuza wezi.
Tuwekeze kwenye kuijenga jamii kwanza. Tuwekeze kwenye kutengeneza mifumo mizuri na kuleta mabadiliko makubwa katika fikra za Watanzania.
Mabadiliko haya hayahitaji bunduki wala mzinga. Hayahitaji polisi wala jeshi na wala hayahitaji vitisho vya aina yoyote ile. Mabadiliko haya yanahitaji elimu na ukombozi wa kifikra, hivyo yanahitaji maongezi, majadiliano na ushirikishwaji.
Ni nani wa kumwelezea Rais wetu ukweli huu? Tukishindwa kuusema ukweli huu tukabaki kuogopa na kutaka kumfurahisha. Tutakuwa tunafanya dhambi kubwa na sote tutaumia. Kulijenga taifa ni mradi wa pamoja ambao ni lazima sote tushiriki bila kutanguliza maslahi binafsi.
Kama ninaruhusiwa kutoa mfano wa mtu ambaye, alilenga kubadilisha mfumo kwanza, kabla ya vitu vingine.
Huyu ni Yesu wa Nazareti. Samahani kwa waumini wa dini nyingine, huu ni mfano wa kutusaidia kufahamu mada hii ninayokazana kuifafanua.
Bwana Yesu anasema hivi:
“Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” (Yohana 17: 21.
Maneno haya ya Yesu, yanaeleweka vizuri ukiyaunganisha na yale ya Yohana 5: 19-20.
“Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya baba, Mwana hukifanya vilevile. Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu”.
Yesu, alikuwa akielezea uhusiano wake na Mungu Baba. Jinsi yalivyo na maisha ya uwazi. Hakuna siri kati yao. Analolijua Mungu Baba, analijua Mungu Mwana, na analijua Mungu roho mtakatifu. Hii ndiyo maana ya Mwana kuwa ndani ya Baba na Baba kuwa ndani ya Mwana na wote wawili kuwa ndani ya Roho Mtakatifu. Wanaishi maisha ya utatu, katika uwazi na kufunuliana. Uwazi huu unawafanya waungane na kuwa kitu kimoja.
Yesu, anatuombea na sisi kuishi maisha ya utatu. Kuishi maisha ya uwazi. Tuwe ndani yake na yeye awe ndani yetu na sote tuwe ndani ya Baba.
Tuwe na familia zenye kuishi utatu. Baba ndani ya familia amjue mama, na mama amjue Baba. Baba ajifunue kwa mama, na mama ajifunue kwa Baba. Kwa njia hii wanaweza kulindana, kuchungana, kuchukuliana na kusaidiana. Ni katika uwazi na kufunuliana familia inaweza kuungana na kuwa kitu kimoja.
Baba na mama wakichukuliana, wakafunuliana, wakalindana na kuchungana, wanajenga mfumo wa kuwalinda na kuwachunga watoto wao. Watoto watakua katika uwazi na kutembea katika mwanga. Watafundishwa maadili mema
Familia zilizoungana na kuwa kitu kimoja, zinatengeneza jumuiya iliyoungana na kuwa kitu kimoja. Jumuiya ikiungana na kuwa kitu kimoja, ni lazima pawepo kufunuliana, kujaliana, kulindana, kuchungana na kusaidiana.
Jumuiya inayoishi hayo niliyoyataja hapo juu, ndiyo inayoweza kupambana na majanga makubwa kama ufisadi na wizi wa rasilimali za taifa letu.
Yote niliyoyasema yanawezekana pale tu ambapo kila mmoja wetu, kila Mtanzania, atasali sala kama ile ya Bwana Sufi Bayazid:
“Nilipokuwa kijana mwanamapinduzi, sala yangu pekee kwa Mungu ilikuwa: ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kuubadilisha ulimwengu’
“Nilipofikisha umri wa mtu mzima na kugundua kwamba sijafanikiwa kuibadilisha roho hata moja, nilibadilisha sala. Nikasema, ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kuwabadilisha watu wanaonizunguka, familia yangu na marafiki zangu’
“Sasa ninapozeeka, bila kufanikiwa kuubadilisha ulimwengu sala yangu imekuwa: ‘Mungu, nipatie nguvu na uwezo wa kujibadilisha mimi mwenyewe’
“Kumbe ningesali hivi tangia mwanzo, nisingepoteza muda wangu bure” (The Song of the Bird – uk 153 – tafsiri ni yangu).
Kama anavyosema Sufi Bayazid, tusiweke nguvu nyingi katika kutaka kuyabadilisha maisha ya wengine, kabla ya kubadilisha maisha yetu sisi wenyewe. Ni kila mmoja wetu kubadilisha maisha yake mwenyewe. Ni kila mmoja wetu kujinyoshea kidole. Kwa njia hii tunaweza kubadilika na kulijenga taifa letu.
Mabadiliko haya ambayo ni muhimu na ni lazima, hayahitaji bunduki na mizinga. Na wala hayahitaji kujenga ukuta. Ni kubadilisha fikra na kusali sala ya Bwana Sufi Bayazid. Mungu, atusaidie kutambua kwamba kulijenga taifa letu la Tanzania ni mradi wa pamoja.
Padre Privatus Karugendo.
pkarugendo@yahoo.co.
+255 754 633122.
No comments:
Post a Comment