Wednesday, September 13

Serikali kuendelea kubana matumizi


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuimarisha mifumo ya udhibiti katika taasisi zake.
Akizindua programu ya marekebisho ya usimamizi wa fedha za umma (PFMRP) jana Jumanne mjini hapa, Samia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha inaboresha mfumo huo.
Samia amewahakikishia wadau wa maendeleo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali katika awamu zilizotangulia zilionyesha mafanikio katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
“Programu hii ilisaidia kuboresha sheria, nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, mipango na michakato ya bajeti na kuanzisha ofisi ya mkaguzi mkuu wa ndani,” amesema.
Amesema programu hiyo itatekelezwa kwa miaka mitano na itaanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha (2017/18) hadi
mwaka 2021/22.
Dk Mpango amesema programu hiyo itahusisha kuweka mifumo thabiti katika kukusanya, kutumia na kugawanya rasilimali ili kusimamia vyema fedha za umma.
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) nchini, Berth Arthy amesema usimamizi mzuri wa fedha za umma ndiyo utawezesha maendeleo kwa wananchi.
“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania siku nyingi, usimamizi mzuri wa fedha za umma ni njia kuu ya kuleta
maendeleo kwa watu tunaowaongoza,” amesema.

No comments:

Post a Comment