Sunday, September 3

Serikali ilivyowafuta machozi wakazi wa Dar na bomoabomoa

Wakazi wa Kimara jiijini Dar es Salaam,

Wakazi wa Kimara jiijini Dar es Salaam, wakosomba tofali juzi baada nyumba za eneo hilo kuvunjwa kwa ajili ya kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro. Picha na Salim Shao 
Amani ya wakazi wanaoishi Bonde la Msimbazi na Toangoma imerejea tena, baada ya Serikali kuwafuta machozi kwa kusitisha ubomoaji wa takribani nyumba 17,300 kwa madai zimejengwa katika maeneo yasiyo rasmi kwa makazi.
Serikali ilieleza kwamba hakuna atakayebomolewa nyumba kwa kuwa wananchi wamemchuagua Rais John Magufuli kwa sababu ya kuwaboreshea makazi na si kuwabomolea.
Serikali ilitoa tamko hilo mbele ya waandishi kwa kuwataka wananchi kuwa na amani kwa sababu nyumba hizo haziwezi kubomolewa kwa kuwa jambo hilo halikufuata sheria.
“Rais ameshangazwa na taarifa ya kubomolewa nyumba 17,000 za Bonde la Mto Msimbazi na 300 za Toangoma,” alisema Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Awali, Baraza la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) lilitangaza kuwa nyumba 17,000 za Bonde la Mto Msimbazi zilitakiwa kubomolewa kwasababu hazipo kwenye makazi rasmi.
Pia, lilieleza kuwa nyumba 300 za Toangoma zikitangazwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa sababu zipo katika hifadhi ya Serikali.
Hata hivyo, Makonda alisema: “Haiwezekani mtu kutoa tamko la kuvunja nyumba 17,000 bila mkoa kujua, hilo haliwezekani.”
Makonda aliwataka wananchi kushiriki kutoa taarifa kwa baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa wanaotumia madaraka vibaya kwa kuwatapeli na kuwauzia wananchi maeneo kinyume na sheria.
Wananchi washindwa kuzuia furaha
Baada ya tamko hilo la Serikali la kusitisha ubomoaji wa nyumba, wananchi walionyesha furaha wakisema kuwa sasa wataishi kwa amani.
Mkazi wa Toangoma aliyejitambulisha kwa jina la Yusuph alisema kauli ya kuwataka kuondoka katika nyumba zao kupisha bomoabomoa iliwatia hofu na kuwakosesha raha.
“Juzi (Agosti 28) DC (Mkuu wa Wilaya ya Temeke) alikuja hapa tukaongea naye, akatuambia tunatakiwa kuondoka, sawa sisi tunakubaliana na agizo hilo lakini hatukua na sehemu ya kwenda na ndiyo maana wakati anaondoka tulimfuata ili atusikilize” alisema.
Alifafanua kuwa hawakuwa na kosa kujenga sehemu hizo kwa kuwa waliuziwa na kiongozi wa Serikali ya mtaa wao, hivyo wanaishi kwa kufuata taratibu zote.
“Hapa ndugu mwandishi tulikuwa tunaishi kama wenzetu wengine wa huko juu, hapa tunalipa kodi ya majengo kama kawaida na hata umeme tulishaomba tuletewe na tumeshawalipa Tanesco,”alisema.
Hata hivyo, alisema agizo la Rais Magufuli kusitisha bomoabomoa limeleta faraja kwao kwa kuwa waliwaza watakwenda wapi.
Mkazi wa Mtaa wa Malela, Annatrophea Raphael alisema kwa sasa ana uhakika na maisha ya familia yake baada agizo hilo la kunusuru nyumba yao kutangazwa na Makonda.
“Mlijionea wenyewe hata kuongea tulishindwa, tena mlivyokuja hapa tulipata uchungu zaidi kwa kuwa tulijua msingeweza kutusaidia chochote ndiyo maana tukawa wakali.
“Leo tumefurahi sana ila tunaomba Serikali iwachukulie hatua viongozi wa Serikali za mitaa matapeli kwa kuwa wao ndiyo walitukosesha amani na kutuweka roho juu,” alisema Raphael.
Hali kama hiyo ilikuwa pia kwa wakazi wa Kigogo baada ya Makonda kutangaza kuwa nyumba zao hazitabomolewa.    

No comments:

Post a Comment