Friday, September 29

Serikali haitavumilia wawekezaji wanaokiuka maadili


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde amesema serikali haitawavumilia wawekezaji wanaokiuka kanuni na taratibu hata kama wanalipa kodi kubwa kiasi gani.
Sanjari na hilo Mhandisi Munde amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wawekezaji wote hasa wa viwanda wasiozingatia taratibu za ajira na kuwanyanyasa wafanyakazi.
Mhandisi Munde ameyasema hayo leo wakati akifunga mafunzo ya siku nne yaliyoandaliwa na asasi ya Social Information and Facilitation yaliyolenga kuwajengea uwezo vijana, kutambua fursa na  kushiriki katika uandaaji na utekelezaji wa sera zinazowahusu vijana.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha   vijana 60  kutoka kata  sita za Mkuranga. Kauli hiyo ya mkurugenzi imekuja baada ya vijana hao kumlalamikia kuwa wanakupangana na vitendo vya unyanyasaji viwandani.
Vijana hao wamedai kuwa licha ya utitiri wa viwanda vilivyopo katika wilaya hiyo havina manufaa kwa kundi hilo.
Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Iddy Sebastian amesema kuwa kuna changamoto kubwa ya ajira katika wilaya hiyo huku vijana wachache wanaopata kazi viwandani wanaishia kuwa vibarua bila mkataba.
"Naomba serikali isikie kilio chetu, tuna viwanda vingi lakini hatunufaiki navyo, wawekezaji wanatunyanyasa, hakuna mikataba ya ajira hivyo vijana wengi wanaishia kukaa majumbani,"
"Zichukuliwe hatua za makusudi ili vijana wa Mkuranga tunufaike na wingi wa viwanda vilivyopo katika wilaya yetu. Niweke wazi kuwa haya mafunzo yamenisaidia kujitambua na nitahamasisha vijana wenzangu wasikate tamaa," amesema Sebastian
Mhandisi Munde alikiri kupokea malalamiko mengi kuhusu waendeshaji wa viwanda na kueleza kuwa serikali inaendelea kuyafanyia kazi.
"Hatutakaa kimya kwa watu wanaokiuka sheria hata kama wanatulipa mabilioni ya kodi. Tumesikia changamoto hizo niwaweke wazi kuwa hatutaruhusu ziendelee kujitokeza," amesema
Aidha Mhandisi Munde aliwaasa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali kwa ajili yao.
Amesema," Kuna fursa nyingi sana, zitumieni. Kuna fedha zinatolewa kwa ajili ya vijana njooni mchukue mzungushe, mrudishe  na wengine wachukue. Lengo la serikali ni kutumia rasilimali tulizonazo kwa ajili ya wanyonge,"

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Hashim Mohamed amesema mafunzo hayo yamesaidia kuwajengea uwezo mpana vijana wa kujitambua na kutambua sera zinazowahusu.

Amesema mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha vijana kutambua na kuchangamkia fursa.

"Wengi walikuwa hawafahamu hata sera ya vijana, nafasi zao kwenye jamii. Tukaona tuwajengee uwezo waweze kupaza sauti na kujitokeza katika masuala yanayowahusu bila woga," amesema Mohamed

No comments:

Post a Comment