Friday, September 29

RIPOTI MAALUM:

Upungufu wa dawa unavyoziweka rehani afya za wakazi Singida vijijini


Tabibu Msaidizi wa Zahanati ya Kinyeto, Godfrey
Tabibu Msaidizi wa Zahanati ya Kinyeto, Godfrey Kiria akimkabidhi dawa Ashura Athuman kwa ajili ya matibabu ya mtoto. Zahanati hiyo iliyopo Kata ya Kinyeto, Wilaya ya Singida Vijijini imekabiliwa na uhaba wa dawa kwa zaidi ya miaka mitatu. Picha na Herieth Makwetta. 
Kinyeto, Singida. Hadija Iddi, mkulima wa Kijiji cha Ntunduu na mwenye umri wa miaka 22, anahaha kupata tiba ya ugonjwa wa kifua unaomkabili mwanaye.
Baada ya kutembea kilomita saba kuifuata zahanati kwenye Kata ya Kinyeto katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida Agosti 7, anakutana na tabibu ambaye anamchunguza bila kuchukua vipimo vya kupeleka maabara kujua tatizo halisi, baadaye anamwandikia dawa moja iitwayo Cough expectorant, dawa inayoondoa makohozi katika njia za hewa.
Anafanya hivyo kwa sababu hakuna maabara ya kuchunguza vipimo kama kohozi, kujua tatizo halisi la mtoto huyo Omary mwenye umri wa miaka miwili.
Hata dawa aliyopewa mgonjwa huyo ni nusu chupa, kutokana na upungufu. Uwezekano wa mama yake kununua dozi kamili katika duka la dawa, ni mdogo kutokana na kutokuwa na kipato cha uhakika.
“Kama sina fedha ya kununua uwele kwa ajili ya uji wa mtoto, nawezaje kuwa na Sh2,500 ya kununua dawa?” anahoji Hadija katika mahojiano na Mwananchi.
“Nitampa hii kidogo niliyopata na ikibidi nitamchemshia majani ya porini, ili kumfukiza yakiwa yanachemka. Hii ni dawa ya asili.”
Hadija ni mmoja kati ya watu 12,082 wa Kata ya Kinyeto wanaokabiliwa na tatizo la uhaba wa dawa katika zahanati hiyo. Vijiji vinne vinavyounda kata hiyo ni Kinyeto, Mkimbii, Minyaa na Ntunduu.
Tatizo hilo limeendelea kudumu licha ya Serikali kutoa kwa asilimia 100 fedha za dawa katika bajeti ya mwaka 2016/17.
Uhaba huo unajitokeza licha ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007 kifungu cha (5.4.3 (c) kubainisha kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau itaimarisha mfumo wa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuzingatia ubora na mahitaji.
Pia, mkataba wa huduma kwa mteja katika sera ya huduma kwa mteja ya Bohari ya Dawa (MSD) kifungu cha 5.5, unasema taasisi hiyo itahakikisha mteja anapata kwa wakati wote dawa muhimu na itasambaza dawa zenye ubora unaokubalika kwa bei nafuu iwezekanavyo.
Mkazi wa Kijiji cha Mkimbii, Abdallah Shumbi ambaye katika umri wa miaka 46 amejaliwa kupata watoto 13, anasema wake zake wawili wamekuwa wakihangaika kutafuta matibabu wanapougua au wanapokwenda kujifungua, lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa  dawa.
“Serikali inatwambia kila mwaka imetenga fedha kwa ajili ya dawa, lakini mbona vituoni hakuna. Tunapohoji viongozi wetu au wabunge kwenye mikutano ya hadhara, wanatwambia tunapaswa kupewa dawa tunazozihitaji, lakini hali ni tofauti,” anasema Shumbi.
Huduma duni kwa wajawazito
Tatizo hilo linawaathiri zaidi wajawazito na watoto.
Siku ambayo Hadija alipata matibabu hayo dhaifu, alikuwapo pia  Saida Ramadhani (19) aliyewasili katika zahanati hiyo akihitaji kujifungua mtoto wake wa pili, hakuwa na kifaatiba chochote.
Pia, Saida hakuwa amemeza vidonge vinavyosaidia kujenga mifupa na kuzuia tatizo la kichwa kikubwa na mgongowazi vinavyojulikana kwa jina la folic acid, wakati wa ujauzito wake. Anasaidiwa kujifungua na mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Joyce Temu kwa kutumia mipira ya kawaida na khanga.
“Tunatumia hii mipira ya kawaida kwa sababu hatuna namna, lakini si salama,” anasema Temu ambaye zahanati yake inahudumia takriban wajawazito 1,350 kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana.
Hali mbaya zaidi ilimkuta Sumaiya Cosma (24), ambaye ana watoto wanne.
“Kuna kipindi hata mipira midogo haikuwapo. Muuguzi alinisaidia kujifungua  kwa kutumia khanga. Nilimuonea huruma na ilikuwa usiku duka la dawa limefungwa, umeme haukuwapo hii inafanya tusijue hatima yetu,” anasema Sumaiya na kuongeza: “Wabunge na mawaziri wanatwambia kila siku mjamzito anapata huduma bure, lakini ukienda kwenye zahanati hakuna vifaa.”
Uhaba wa dawa si tatizo pekee katika zahanati hiyo, bali hata chanjo za kuzuia magonjwa.
“Tumehoji kwenye mikutano, lakini tunaambiwa kinachofanya dawa zipungue ni wagonjwa wa CHF kuwa wachache. Sasa wameongezeka bado hali inasuasua,” anasema mkazi wa Kijiji cha Kinyeto, Zainab Kisaka.
Wahudumu hutumia vifaatiba hivyo visivyo rasmi  kwa kuwa vifaa kutoka MSD haviwafikii kwa wakati.
Akizungumzia suala hilo, Temu anasema mwaka wa fedha uliomalizika kulikuwa na upungufu wa dawa hasa za viua vijisumu (antibiotic), dawa za maji za watoto, vifaa na vitendanishi hasa vya kupimia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), glovu na paracetamol ya kutuliza maumivu.
Hata hivyo, Temu anasema shehena ya dawa walizopata kwa robo mwaka, imetosheleza kidogo.
Zahanati hiyo inaweza kupima malaria, HIV na mkojo kung’amua maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).
“Dawa zikiadimika, zahanati hutuma maombi kwa Daktari wa Wilaya (DMO) ambaye hununua kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF),” anasema.
“Tukiishiwa huwa tunakwenda kuchukua dawa zahanati nyingine za karibu kama Mramo na kama zitakosekana kabisa, ndiyo tunamwandikia mgonjwa dawa ili aenda kutafuta sehemu nyingine. Lakini kwa mfumo wa sasa, huwa tutaanza kununua kwa kutumia fedha zetu.”
Kiini cha upungufu wa dawa
Kuhusu sababu za upungufu wa dawa, Temu hasiti kuinyooshea kidole MSD.
“Mwezi Mei zahanati iliomba dawa aina 82 ambazo ni muhimu, lakini ilipata aina 36 pekee,” anasema Temu.
Hati ya malipo ya Mei iliyopokelewa Juni 28 ambayo mwandishi gazeti hili ameiona, inaonyesha zahanati hiyo ilipata dawa aina 35 kati ya 81.
“Tulipohoji tuliambiwa hazipo stoo,” alisema Temu na kuongeza: “Juni 28 tuliletewa dawa zenye thamani ya Sh1.8 milioni. Kwa  sasa akaunti yetu ina Sh6.5 milioni kwa hiyo unakuta kwenye akaunti tunazo fedha nyingi, kuna upungufu wa dawa.  MSD ndiyo hawana dawa si kwamba akaunti haina fedha.”
Kauli za viongozi
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida (DMO), Dk Sungwa Kabissi anasema kuna upungufu wa vitendanishi na kwamba, kuna aina za dawa zinaweza kukosekana kwa sababu hazihusiki kwenye zahanati.
“Kwa sasa tunaangalia namna tunavyoweza kuisaidia zanahati hiyo kununua dawa na vifaatiba vilivyopungua, kwa kutumia fedha kidogo walizonazo,” anasema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Singida, Rashid Mandoa anasema kwa sasa upungufu wa dawa unaainishwa kutoka kituo husika, kama ni zahanati, kituo cha afya au hospitali baada ya kamati za afya kuainisha, ina  uwezo wa kununua dawa moja kwa moja kwa kuwa Serikali inawapelekea fedha.
Hata hivyo, Mandoa anasema changamoto kubwa ni zahanati kutotaka kununua dawa kwao na wanafuatilia suala hilo.
Uongozi wa MSD unasema hali inayozungumziwa katika Zahanati ya Kinyeto ni ya mwaka uliopita wa fedha na kwamba, matatizo hayo yalishashughulikiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu anasema Kinyeto walipelekewa dawa walizokosa wakati huo kwa huduma ya marudio ya kukamilisha maombi yao ili wapate dawa.
“Bidhaa nyingine chache zilizosalia tayari zimeshaagizwa kutoka kwa wazalishaji na zinategemewa kuingia nchini kuanzia wiki ijayo,” anasema Bwanakunu na kuongeza:
“Hivyo, tutasambaza dawa Halmashauri ya Singida Mjini, Vijijini na Ikungi na mizigo imeanza kupakiwa na itafikishwa kuanzia Agosti 28.”
Gazeti hili lilirudi Kinyeto Septemba 16 na kukuta zahanati hiyo ikiwa na dawa zote zilizokuwa zimekosekana awali.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anafahamu upungufu uliopo na kueleza kwa sasa hali ya upatikanaji  dawa muhimu nchini unaridhisha.
 “Si sahihi kusema kuna upungufu wa dawa, hiyo ni historia ya mwaka wa fedha 2015/16,” anasema Waziri Ummy na kuongeza:
“Katika sekta ya afya, moja ya mambo makubwa ambayo Serikali  imeyafanya ni kuimarisha upatikanaji dawa. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa wananchi wanapaswa kuchangia ili kupata huduma za matibabu.”
Anasema kazi iliyo mbele kwa sasa ni kuhimiza wananchi kujiunga na bima ya afya, ili kuwezesha upatikanaji matibabu bila kikwazo.
Alipoulizwa kuhusu malengo ya Ilani ya CCM ya kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata na kuzipa vifaa, dawa na watumishi, Waziri Ummy anasema wataendelea kushirikiana na Ofisi ya Tamisemi kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Anaisema mkakati huo ni kuhakikisha Serikali inapeleka watumishi, fedha za dawa, vifaa na vifaatiba na kupeleka fedha za uendeshaji.
Inaonekana upungufu huo husababishwa na udhaifu katika usimamizi, upangaji na usafirishaji dawa, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa na Serikali la Sikika, Irinei Kiria.
“Pia, inategemea namna ambavyo wahusika wa kituo wanafuatilia; viongozi wa wilaya wanavyosimamia na wanahakikisha vipi dawa ambazo zipo kwenye ghala la MSD zinafika vituoni mwao,” anasema Kiria na kuongeza: “Utafiti tunaofanya tunashuhudia maeneo mengine yana dawa kwa asilimia 100 na kwingine mpaka asilimia 50. Kuna tofauti kubwa.”

No comments:

Post a Comment