Friday, September 29

Rahco yalegeza masharti ya bomoabomoa Tanga, D’Salaam na Kilimanjaro


Kuna wakazi ambao wamejenga pembezoni mwa njia ya reli katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam watakaokuwa wanachekelea hivi sasa baada ya kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kulegeza masharti ya umbali kwa majengo yanayopaswa kubomolewa.
Wakazi waliokuwa wakikabiliwa na bomobomoa hiyo katika miji ya Tanga na Moshi walifikisha vilio vyao kwa wakuu wa mikoa yao, Martine Shigela na Anna Mghwira, mtawalia, ambao walitoa maagizo ya kutumika kwa busara na mazungumzo kufikia muafaka wa suala hilo.
“Tanga barabara nyingi zinakutana na reli kwa hiyo tungeamua kufuata sheria ( ya mita 100) wengi wangeathirika. Kwa hiyo tuliamua kutumia umbali wa mita 30 kila upande,” alisema Ofisa Habari wa Rahco, Catherine Moshi alipohojiwa kwa simu jana na kuongeza kuwa hatua hiyo pia imechukuliwa kwa mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam.
“Kuna maendeleo mengi yamefanyika baada ya maeneo ya reli kuchukuliwa, huku baadhi ya halmashauri zikiuza maeneo ya reli. Siyo Tanga tu, Moshi pia tuliona tuache kutumia sheria hiyo. Hata Dar es Salaam kama tungeamua kubomoa maeneo ya Kamata wengi wangathirika, ndiyo maana tukarudi kwenye mita 30 tu,” alisema.
Hatua ya nyumba zilizo ndani ya mita 100 katika maeneo yenye barabara zinazokutana na reli mkoani Tanga kuwekewa alama ya X ilitia kiwewe wananchi na kumfanya Shigela kuingilia kati akiiomba Rahco kutumia busara.
Mbali na Shigela, Mghwira naye alimwagiza mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Moshi, kufanya mazungumzo na Rahco kuepusha bomoabomoa eneo la Pasua.
Moshi alisema maeneo mengi ya reli yalimegwa na kuuzwa na halmashauri na manispaa hasa wakati shirika hilo lilipoingia ubia na kampuni ya Rites ya India mwaka 2007 wakati shughuli za kuendesha usafiri wa reli zilipohamishia katika shirika jipya la Tanzania Railways Limited (TRL), na Serikali ikaunda Rahco ili kusimamia wa rasilimali za reli.
Hata hivyo, mwaka 2011 Serikali ilichukua tena hisa zote za TRL.
“Uzembe ulikuwepo wakati ule. Maeneo mengi yalichukuliwa na wao (Rites) hawakujali kwa sababu hakikuwa kipaumbele chao,” alisema Moshi.
Alisema Sheria ya Reli inatambua mita 30 kila upande kuwa mali ya shirika hilo huku pia kukiwa na mita 100 kwenye maeneo ambayo reli imekutana na barabara.
“Kilichotokea Tanga ni maeneo ya reli yanayokutana na barabara yanayoitwa ‘Diamond crossing’ yanayotaka kuwe na mita 100, ndipo mkuu wa mkoa alipoomba busara itumike.”
Alisema eneo la mita 30 kila upande wa reli linaitwa corridor lakini pia kuna maeneo ya vituo vya reli ambayo umbali ni mkubwa zaidi, “Kuna maeneo mengi ya reli yamevamiwa ndiyo maana tunabomoa. Maeneo ya stesheni ni makubwa zaidi hata zaidi ya mita 120, hayo hatutakubali yachukuliwe,” alisema.

No comments:

Post a Comment