Friday, September 29

CDA yaiachia Halmashauri Dodoma deni la Sh16.3bn


Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma itatakiwa kufanya kazi ya ziada kulipa watu na taasisi zilizokuwa zinaidai Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) baada ya kuachiwa fedha zisizolingana na madeni.
Rais John Magufuli aliivunja CDA Mei 15 na kuitaka ikabidhi mali na madeni yote kwa manispaa hiyo.
Lakini taarifa ya mali na madeni ya CDA inaonyesha kuwa Manispaa ya Dodoma itakuwa na mzigo mzito wa kukabiliana na deni la Sh16.3 bilioni la mamlaka hiyo.
Katika kikao cha dharura cha baraza la madiwani ambacho kilipokea taarifa ya mali zilizokabidhiwa na CDA, mweka hazina wa manispaa hiyo, Alfred Mlowe alisema deni hilo ni la hadi kufikia Mei 15.
Lakini alisema hadi kufikia Mei 17, akaunti mbalimbali za mamlaka hiyo kama ya NMB, CRDB na Benki Kuu (BoT) zilikuwa na jumla ya Sh12.4 bilioni huku fedha taslimu zikiwa ni 13.5 milioni pekee.
Alisema wanachama 77 wa THTU wa Chuo Kikuu cha Dodoma wanadai Sh90 milioni, pamoja na deni la fidia ya ardhi na mali kwa wananchi (Sh1.4 bilioni), matazamio ya kazi (Sh125 milioni) na fedha za maboresho na kodi ya nyumba zilizolipwa Sh82.6 milioni. Madeni mengine ni Sh37.2 milioni za michango ya hifadhi ya jamii, watumishi na watoa huduma (Sh483 milioni), CRDB (Sh6.4 milioni) na deni linaloweza kujitokeza kutokana na kesi zilizoko mahakamani, Sh1.2 bilioni.
“Mapendekezo ya vikosi kazi vya uhakiki vilivyoundwa na Wizara ya Fedha ni kutaka halmashauri kutumia fedha iliyobaki kuwalipa wadeni wa CDA ikiwa ni pamoja na hati za malipo zilizoandaliwa na hundi kuandikwa lakini hazikulipwa kutokana na akaunti za benki kufungwa,” alisema.
Kuhusu wadaiwa, Mlowe alisema CDA ilikuwa ikidai Sh13.1 bilioni hadi ilipokuwa inavunjwa, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa viwanja 1,006, kodi ya ardhi, nyumba, tozo ya minara ya mawasiliano na mradi wa nyumba za gharama nafuu.
Alisema Manispaa ya Dodoma imekabidhiwa mali mbalimbali ikiwa ni pamoja na magari, majengo na ardhi ambavyo vina thamani ya Sh68.3 bilioni.
Akizungumzia mzigo huo, Diwani wa Majengo (CCM), Mayaoyao Msinta alishauri kuomba msaada Serikali Kuu kulipa madeni hayo kwa kuwa baadhi hayalipiki.

No comments:

Post a Comment