Tukio hilo lilitokea jana Jumapili ofisa huyo alipokwenda kuangalia utekelezaji wa agizo alilotoa Agosti 27 la kuwapa siku 14 wakulima hao wawe wameondoka katika bwawa hilo.
Ofisa huyo amesema alienda eneo hilo akiwa amefuatana na baadhi ya viongozi wa mtaa kukagua iwapo wakulima wameondoka lakini waliwakuta wakiendelea na kilimo kwenye vyanzo vya maji.
“Nilipofika eneo hilo nilikuta wakulima zaidi ya 19 wakiendelea na kilimo, baadhi wakipanda nyanya na mahindi. Nilianza kuwapiga picha kupata ushahidi, walipobaini walinishambulia kwa fimbo huku viongozi niliofuatana nao wakitimua mbio,” amesema ofisa kilimo Issa.
Amesema baada ya kuanguka, wakulima walitimua mbio na majembe yao na fahamu zilipomrudia alienda kituo cha polisi kuchukua fomu kwa ajili ya matibabu ambayo aliyapata katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga na aliruhusiwa kurejea nyumbani.
Hata hivyo, amesema hataogopa kufanya kazi na kuwachukulia hatua wote watakaoendelea kulima kwenye vyanzo vya maji.
Mtendaji wa Kata ya Igunga, Robert Mwagala amesema Polisi kwa kushirikiana na raia wema watawasaka wakulima waliomshambulia ofisa kilimo huyo.
Diwani wa Igunga, Charles Bomani amesema kitendo kilichofanywa na wakulima hao hakikubaliki, hivyo ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Baadhi ya wakulima waliotii agizo la kuondoka kwenye bwawa hilo wamelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka juu ya watu waliofanya ukatili huo.
Mkazi wa Kata ya Igunga, Idd Jackson amesema ni aibu na fedheha kumshambulia kiongozi akitekeleza majukumu yake, hivyo ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe kwa waliohusika.
No comments:
Post a Comment