Monday, September 11

Mbunge ataka Spika ateue ujumbe kwenda kumjulia hali Lissu


Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Jaku Hashim Ayoub ameomba mwongozo wa Spika akitaka Bunge liteue wabunge wa kwenda kumuona mwenzao wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayepata matibabu mjini Nairobi, Kenya baada ya kujeruhiwa kwa risasi.
Lissu alijeruhiwa Septemba 7 akiwa ndani ya gari nyumbani kwake Area D mjini hapa na alisafirishwa siku hiyohiyo kwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi. Awali, alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza baada ya kipindi cha matangazo ya wageni bungeni leo Jumatatu, Jaku amesema Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alifanya kitendo cha kibinadamu kuruhusu gari la ndugu zake limpeleke Lissu hospitali.
Amesema kwa ubinadamu, anaomba mwongozo wa Spika wateuliwe wabunge kwenda kumuona Lissu.
Dk Tulia akijibu mwongozo huyo amesema wapo wabunge Nairobi ambao humletea taarifa Spika kila wakati juu ya hali ya mbunge Lissu.
Amewataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na  Mwenyekiti wa Chadema, pia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Mwingine ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

No comments:

Post a Comment