Thursday, September 28

Nusu ya Watanzania hawajui fedha wanazotumia kwa wiki

Dar es Salaam. Licha ya kuongezeka kwa wananchi wanaotumia huduma za fedha nchini, utafiti unaonyesha nusu ya watu wazima hawafahamu kiasi cha fedha walichotumia wiki iliyopita.
Matokeo ya utafiti wa awamu ya nne wa Financial Sector Deepening Trust (FSDT) yaliyotolewa leo Alhamisi yanaonyesha watumiaji wa huduma za fedha nchini wameongezeka kutoka asilimia 58 miaka minne iliyopita hadi asilimia 65 mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha, "Asilimia 50 hawafahamu fedha wanazotumia kwa wiki moja iliyopita."
Kuongezeka kwa wanaopata huduma za fedha bado hakujawasaidia wananchi wa vijijini ambako masikini na wakulima wengi wanapatikana.
Wakati zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wakiishi vijijini na kutegemea kilimo kwa kipato chao, ni asilimia tatu pekee wana hatimiliki za ardhi waliyonayo.
"Hii inawafanya wakose mikopo hasa kutoka taasisi zinazohitaji dhamana," inasema taarifa hiyo.
Kutokana na kutokuwa na uhakika wa kipato, asilimia 56 ya wananchi 10,000 walioshiriki utafiti huo walisema hupunguza matumizi yao wanapohisi kuishiwa.
Utafiti huo ni wa nne ikiwa ni zaidi ya miaka 10 tangu ulipotolewa wa kwanza mwaka 2006 ukifuata mwingine mwaka 2009 na 2013.

No comments:

Post a Comment