"Migogoro mingi ya Ardhi ni kutokujituma kwa watu wetu" RC Gambo
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo wakati anahitimisha mkutano wake na wananchi wa wilaya ya Karatu wenye kero mbalimbali za Ardhi,Nyumba na Makazi.
"Toka nianze mikutano mikutano hii na wakazi wa Jiji la Arusha na leo nipo hapa Karatu migogoro mingi si mikubwa kama inavyoonekana bali inachangiwa na uzembe wa watu wetu katika mabaraza ya Ardhi na mahakama kutokutimiza wajibu wao ipasavyo" alisema Gambo.
Katika mikutano hiyo maalum ambayo mkuu huyo wa mkoa ameshaifanya katika jiji la Arusha na Karatu amekutana na migogoro mingi ambayo kiuhalisia imeshasuluhishwa katika hatua mbalimbali za kimaamuzi lakini wananchi hao hawajapewa mrejesho.
"Tatizo letu sisi watendaji ni kutokuwaandikia watu hawa wa nini tumekifanya katika maamuzi yetu na kutokuweka kumbukumbu sahihi, kama mmeshughulikia tatizo la mtu mpeni mrejesho kwa maandishi na kama ataona hajaridhika mshaurini hatua zaidi za kufuata na jambo hilo liwekwe kwenye kumbukumbu zetu ili akija wakati mwingine tusipate shida kwa kudhani ni jambo jipya" alisisitiza Mhe Gambo.
Vilevile amemuagiza Kamishna wa Ardhi kutuma timu maalum itakayoshughulikia kero hizo ndani ya muda mfupi na kuyafanyia ukaguzi mabaraza yote ya Ardhi wilaya za Arusha mjini na Kararu.
"Kamishna nitakutana mara baada ya ziara ya mwenge kupita mkoani mwetu ulete timu maalum itakayopiga kambi hapa kumaliza kero hizi kwani hapa kuna wengine wala hawana migogoro ya ardhi bali wamevamiwa kwenye maeneo yao watu kama hawa polisi ndio sehemu husika na sio kwenye mabaraza ya ardhi, vilevile ukayafanyie ukaguzi mabaraza ya Ardhi ya Arusha mjini na Karatu kwani nayo sioni kama wanafanya kazi zao sahihi sana" aliagiza mkuu huyo wa mkoa.
Katika mikutano hiyo maalum aliyoianza tarehe 29/08/2017 kwa Jiji la Arusha na tarehe 30/08/2017 kwa wilaya ya Karatu Mkuu huyo wa mkoa ameambatana na wataalam wa Ardhi toka ofisi ya Kamishna wa Ardhi,Msajili wa hati Kanda, wataalam wa Ardhi mkoa wa Arusha, mwanasheria toka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali na wataalam mbalimbali toka halmashauri husika.
Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kua na migogoro mingi ya Ardhi na ya muda mrefu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo(katikati) akiendesha mkutano wa kuwasikiliza wanachi wa Jiji la Arusha kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Fabian Daqqaro na kulia ni Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bwana. Chitukuro .
Baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha wakisubiri kumuona mkuu wa mkoa wa Arusha na kumweleza kero zao
Wananchi wa wilaya ya Karatu wakiwa katika makundi kusubiri kuonana na RC Gambo na kutoa malamimiko yao.
No comments:
Post a Comment