Friday, September 15

Mazoezi ya kijeshi ya Urusi na Belarus yaanza na kuzua hofu Ukraine

Russian tank (file pic)Haki miliki ya pichaMIL.RU
Image captionKifaru cha Urusi kikielekea kwa mazoezi ya kijeshi ya Zapad
Urusi na Belarus zimeanza mazoezi makubwa ya pamoja ya kijeshi, ambayo yamepewa jina Zapad-2017, na ambayo yamezitia wasiwasi nchi jirani wanachama wa shirika la kujihami la nchi za Magharibi la Nato.
Mazoezi hayo ni moja ya mazoezi makubwa kabisa ya kijeshi kuwahi kufanywa na Urusi tangu ilipotwaa rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wanajeshi 12,700 wanashiriki, lakini wataalamu wa Nato wanatarajia kwamba idadi itakuwa juu zaidi ya hiyo.
Mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika ndani na maeneo ya karibu na belarus na yanashirikisha vifaru, ndege za kivita na manowari.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameonya kuwa Zapad-2017 (jina ambalo maana yake kwa Kirusi ni "Magharibi") huenda ikawa ni hatua ya mwisho kabla ya kuivamia Ukraine.
Kiev imeimarisha ulinzi wake mpakani.
Makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo makubwa ya mashariki mwa Ukraine na wameendelea kukabiliana na wanajeshi wa serikali.
Hii ni licha ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano Februari mwaka 2015 mjini Minsk.
Nato imeituhumu Urusi kwa kuwapa waasi hao silaha kalikali pamoja na wanajeshi.
Urusi imekanusha tuhuma hizo, lakini imekiri kwamba kuna baadhi ya raia wa Urusi "wanaojitolea" wanaowasaidia waasi hao.
Nato imetuma wanajeshi jumla ya 4,350 Poland, Estonia, Latvia na Lithuania, nchi ambazo zinapakana na Belarus na Urusi.
Nchi 29 wanachama wa Nato pia zinashika doria angani katika mataifa ya eneo la Baltic.
Zapad
Kinachofanyika wakati wa mazoezi ya sasa ya kijeshi ya Zapad-2017 ni kuigiza hali dhahania ya maasi nchini Belarus ikiongozwa na "wasaliti" na "magaidi" wanaoungwa mkono na nchi dhahania kwa jina "Veishnoria".
Wanajeshi wa Urusi wanatumwa Belarus kuisaidia kumaliza maasi hayo.
Lengo kuu ni jinsi ya kuunganisha makao makuu ya kijeshi ya mataifa hayo mawili wakati wa vita.
Belarus imetuma wanajeshi 7,200 na Urusi imetuma wanajeshi 5,500, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.
Jimbo la Urusi la Kaliningrad - ambalo lipo katikati ya Poland na Lithuania ambazo ni nchi wanachama wa Nato - limeshirikishwa katika mazoezi hayo ya kijeshi.
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ana uhusiano wa karibu na Urusi, ingawa kumekuwepo na mzozo wa mara kwa mara kati ya serikali yake na Urusi kuhusu biashara.

No comments:

Post a Comment