Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imesema imetenga eneo la Kibada wilayani Kigamboni kwa ajili ya maduka hayo kwa magari mapya na yaliyotumika.
Eneo hilo kwa ajili ya mauzo ya magari makubwa na madogo litaanza kutumika Januari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Akizungumza na wadau na wafanyabiashara wa magari ofisini kwake leo Ijumaa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema wameamua kutenga eneo moja la kuuzia magari kwa kuwa kufanya hivyo kuna faida kuu tatu.
Amesema faida ya kwanza ni mwananchi kuwa na uwezo wa kununua gari sehemu moja na akapata nafasi ya kuchagua analolipenda kwa kadri awezavyo katika eneo moja.
“Ukiwa sehemu moja ni rahisi kufanya uamuzi baada ya kuona ubora wa gari au magari unayotaka,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema faida ya pili ni kwa wafanyabiashara wa magari kuonyesha bidhaa zao kwa wateja wanaowafikia katika eneo la soko na hakutakuwa na kificho kama ilivyo sasa.
Amesema faida ya tatu ni kuiwezesha Serikali kukusanya kodi kwa ufanisi kwa kuwa kutakuwa sehemu moja na huduma zote zikiwemo za bima na namba za magari zitakuwa zikipatikana katika eneo hilo ambalo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watakuwepo.
No comments:
Post a Comment