Friday, September 1

Kesi ya Urais nchini Kenya, maamuzi leo

Rais Uhuru Kenyatta
Image captionRais Uhuru Kenyatta
Mahakama kuu nchini Kenya leo itatoa uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na Muungano wa Upinzani nchini humo wa kupinga Uhuru Kenyatta, kutangazwa tena kuwa mshindi wa Urais.
Muungano huo wa NASA unadai kuwa matokeo ya uchaguzi ya mwezi Agusti yalikuwa na udanganyifu.
Tume ya taifa ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi kwa ushindi wa zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa na kumshinda mpinzani wake mkubwa, mkongwe wa siasa za upinzani Raila Odinga.
Muungano wa upinzani nchini Kenya unaitaka mahakama kuu kubatilisha matokeo hayo ya uchaguzi wa mwezi uliopita.
Unadai kuwa mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa. Upinzani pia unaituhumu Tume ya taifa ya Uchaguzi kwa kutumia namba za kupigia kura ambazo zilikuwa hazijathibitishwa rasmi.
Mahakama inayosikiliza kesi hiyo imeruhusu tayari mawakili wa upinzani kuweza kupata Data na vifaa vilivyotumika katika uchaguzi.
Kenya ilianza kutumia mfumo wa kidigital katika mchakati wake wa uchaguzi, baada ya mgogoro uliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2007, uliosababisha kutokea kwa ghasia.
Lakini mfumo huo mpya wa kielectroniki ulishindwa kufanya kazi katika uchaguzi uliofuata wa mwaka 2013 na kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema mfumo huo umeshindwa tena.
Na iwapo upinzani utashinda katika kesi hii, uchaguzi utabatilishwa na mwingine mpya utafanyika ndani ya siku 60.
Lakini kama hali itabaki kuwa hivyo, Rais Kenyatta anaelekea kupata changamoto kubwa kuweza kuliunganisha tena taifa hilo lililogawanyika kisiasa.

No comments:

Post a Comment