Hayo yamesemwa leo Jumatano na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Kabla ya Hakimu Mkeha kusema hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alieleza kuwa mara ya mwisho waliomba siku 14 ili waweze kuelezea hali ya upelelezi ulipofikia lakini wameshindwa hivyo wakaomba kuongezewa muda ili tarehe ijayo waweze kueleza.
Alieleza kuwa wanafanya jitihada kuona upelelezi unakamilika na akaomba tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Baada ya Kishenyi kueleza hayo, wakili wa utetezi, Masumbuko Lamwai alidai kuwa kesi ilifikishwa mahakamani hapo Aprili Mosi, 2016, hivyo ni karibu mwaka mmoja na nusu sasa, mashtaka yanayowakabili wateja wake yanahusisha nyaraka ambazo wanazo na kwamba hakuna uchunguzi nje ya nyaraka.
Wakili Lamwai amesema walikuwa wakilalamikia kesi ya utakatishaji fedha kuwa imewekwa kwa makusudi ili wateja wao wakae gerezani.
"Kwa mtu anayekaa gerezani kwa mwaka mmoja na nusu, kuambiwa upelelezi bado haujakamilika inaleta mshangao.
"Hii kesi imekuwa kama ya kukomoana komoana hivi, mheshimiwa wateja wetu ni watu wazima wanashughuli zao na nyingine zimefilisika kwa kukosa usimamizi," ameeleza Wakili Lamwai mahakamani hapo.
"Tunajua mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi hii lakini upande wa mashtaka wanatumia vibaya taratibu za kimahakama."
Baada ya kutolewa kwa maelezo ya pande hizo zote mbili, Hakimu Mkeha amewaambia washtakiwa kuwa upelelezi unaofanywa unakaribia mwisho akaomba wawe na imani, kwa kuwa amejiridhisha yeye mwenyewe kwa macho yake kuwa upelelezi unakaribia kufika mwisho.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 5, 2017. Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola milioni 6 za Marekani.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani 550 milioni kwa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Uingereza.
No comments:
Post a Comment