Friday, September 15

Ecobank yaangazia mageuzi ya teknolojia

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba
Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee(kushoto) akiwa katika mahojiano maalumu leo katika ofisi za Mwananchi. 
Dar es Salaam. Benki ya Ecobank imeanzishakwa mara ya kwanza huduma ya malipo mtandaoni yanayohusu viza na Mastercard bila kutumia kadi kupitia programu ya simu.
Uanzishwaji wa huduma hiyo ni sehemu ya mikakati ya benki hiyo kuhakikisha inawafikia wateja wengi zaidi na kuwarahisishia kufanya biashara kwa kuwaruhusu kufanya miamala katika maeneo tofauti duniani.
Mkurugenzi mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee amesema jana Alhamisi kuwa, huduma hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo itakuwa sehemu ya uboreshaji wa programu ya sasa ya Ecobank mobile app ambayo inarahisisha ufanyaji miamala kutoka na kwenda benki na akaunti za fedha za simu.
Mzee amesema huduma hiyo itawasaidia zaidi wateja ambao katika maeneo walipo hakuna uwezekano wa kufanya malipo kwa kutumia akaunti ya benki ya simu na hasa nje ya nchi.
“Huduma itakayopatikana kwenye Ecobank mobile app ni salama na inakidhi vigezo vyote vya kufanya malipo kimataifa. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wameshaithibitisha, tuliwapelekea nyaraka zote na kuwaonyesha huduma inavyofanya kazi na kitengo cha usimamizi kimeridhia,” amesema.
Mzee aliyeanza kuiongoza benki hiyo Julai mwaka huu, amesema mipango yao ni kuhakikisha wanawekeza katika huduma za digitali katika kiwango kikubwa kwa wateja wote.
“Lengo letu ni kuwapatia wateja urahisi wa kupata huduma za kibenki ili hata kama mtu ana kazi nyingi afanye muamala kwenye simu akiwa anakula chakula cha mchana,” amesema Mzee katika mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) jana.
Amsema “Tunataka kupunguza matumizi ya fedha taslimu kwa sababu uhalifu ni mwingi siku hizi.”
Mbali na uwekezaji wa huduma za kidigitali, amesema wamepanga kuongeza wateja, mtaji na kukuza faida kwa wanahisa wake.
Ecobank ni benki ya kimataifa inayopatikana katika nchi 36 barani Afrika na baadhi ya maeneo ya Uingereza, Ufaransa, Dubai na Beijing nchini China.
Mzee ambaye benki yake ipo katika kundi la pili la benki (Tier 2), amesema wataendelea kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa kutoa mikopo itakayosaidia wafanyabiashara kufikia malengo yao na hasa biashara zinazovuka mipaka na uuzaji wa mazao.
Katika mikakati ya sasa ya kuimarisha benki hiyo ambayo katika robo ya kwanza ilikuwa na mikopo chechefu kwa asilimia 57 ya mikopo yote, Mzee amesema wana mpango wa kuanzisha mikopo ya nyumba, mikopo inayotokana na dhamana ya mishahara na mingineyo.
Mikopo chechefu ni ile ambayo haijalipwa baada ya kuilipa kupita na kufanya ionekane hailipiki.
“Tunataka kuongeza wigo wa huduma zetu wa kuangazia sekta kama vile huduma ndogondogo za benki, asasi za kiraia, Saccos na shule. Tunataka tuwe vinara katika sehemu hii ya huduma,” amesema Mzee na kuongeza moja ya kazi kubwa atakayoifanya ni kupunguza mikopo chechefu.
Katika mahojiano hayo maalumu, Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu amemweleza Mzee kuwa kampuni  inawekeza kwa kiwango kikubwa katika digitali ili kuhakikisha habari zinawafikia watu wengi zaidi na kwa haraka.
MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na mtandaoni kupitia MCL Digital.

No comments:

Post a Comment