Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limesema kwamba kesho litaungana na viongozi wa kiroho kufanya maombi maalum dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Baraza hilo limesema hayo ni maombi ya Kitaifa ya Vijana Kumuombea Tundu Lissu ambaye hali yake bado si nzuri, akiwa chumba cha uangalizi maalum, Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Katibu Mkuu wa baraza hilo ,Julius Mwita maombi hayo yanatarajiwa kufanyika Jumapili, Septemba 17, katika Uwanja wa Tip, Sinza darajani, jijini Dar es Salaam.
‘’Kupitia Kamati ya Maandalizi, Bavicha inapenda kuwaambia Watanzania wote ambao watapenda kuhudhuria maombi hayo kuwa maandalizi yote muhimu yameshafanyika kwa ajili ya kuhakikisha shughuli hiyo ya kiimani inafanyika kama ilivyopangwa’’ imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Ameongeza kwamba ‘’Hadi sasa tumezingatia taratibu zote za kisheria ambazo zinatuelekeza kutoa taarifa kwa mamlaka za kiserikali, hususan Jeshi la Polisi’’Amesema kwenye taarifa hiyo
Mwita amesema hadi sasa polisi hawajaandikia barua ya kuwata ili kujadiliana nao kuhusu kufanikisha shughuli hiyo, hivyo wanaamini kuwa hawana pingamizi lolote la kiutaratibu kama ambavyo sheria inaelekeza.
Amesema wamefuatilia kwa kina kuhusu kauli za Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambazo zimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo ikidhaniwa kuwa amezuia shughuli hiyo ya maombi.
Amesema wamebaini kuwa Kamanda Mambosasa hakueleweka vyema, kwa sababu aliulizwa swali kuhusu shughuli yao ya kumuombea Lissu, lakini yeye akatoa majibu kwa kuzungumzia maombi ya maandamano ya watu walioomba kibali cha kuwapokea wabunge wao wakiwa wanatokea Dodoma, ndiyo maana akazungumzia maandamano.
‘’Tumejiridhisha tena kuwa taarifa tuliyopeleka Polisi kama sheria inavyoelekeza, tukiwataarifu kuhusu maombi hayo, haikutaja wala kuzungumzia maandamano bali watu wa dini mbalimbali zilizopo nchini wanaoguswa na tukio la Lissu na maumivu anayopitia hospitalini, watakutana na kuomba sala/dua ili Mwenyezi Mungu afanye uponyaji kwa mgonjwa wetu’’ amesema Mwita
Amesema kwamba Bavicha wamefanya kazi ya kuratibu tu maombi hayo, lakini itakuwa ni shughuli ya kiimani, ndiyo maana wamealika viongozi wa kiroho waje kusimamia na kuendesha maombi hayo ya kumuombea Lissu.
‘’Kwa wito huu, tunawasihi na kuwaomba watanzania wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuja kumuombea ndugu, rafiki, mwanachama na kiongozi wetu Lissu, pamoja na taifa kwa ujumla’’ amesema
No comments:
Post a Comment