Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema mchango wa Cuba katika kuimarisha afya za wananchi wa Bara la Afrika unaimarika kila siku kutokana na misingi imara ya ushirikiano wa karibu na kiundugu ulioanzishwa na muasisi wa taifa hilo Fidel Castro Balozi Seif ameyasema haya Leo mjini Havana wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Afya ya umma mheshimiwa Roberto Morales Ojeda.
Amesema kutokana na uhusiano mzuri na kiundugu uliopo kati ya Tanzania na Cuba, Zanzibar imeweza kutoa madaktari wasiopungua 50 ambao wamefundishwa na madaktari kutoka Cuba. Amesema kupatikana kwa madaktari hao kumeiweka Zanzibar nafasi nzuri ya kufikia malengo yake ya kuwa na kituo cha afya chenye daktari kwa kila kilometa nne.
Balozi Seif ameiomba Serikali ya Cuba kuipatia Zanzibar madaktari 3 mabigwa katika fani ya figo (Nephrologist); masikio, pua na koo (ENT) na mionzi (Radiologist). Aidha ameitaka Cuba kuwapatia vijana waliomaliza mafunzo ya udaktari chini ya madaktari wa Cuba nafasi za mafunzo ya juu katika fani mbali mbali.
Naye Waziri wa Afya ya umma mheshimiwa Roberto ameeleza kuridhishwa kwake na uhusiano ulipo wa sekta ya afya kati ya Zanzibar na Cuba. Amesema Cuba iko tayari kuwapatia mafunzo ya juu vijana wa Zanzibar kwa gharama nafuu na kuitaka Wizara ya Afya ya Zanzibar kupeleka maombi yake mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa wataalamu wa Afya Waziri wa Cuba Mheshimiwa Roberto amesema Serikali yake itarifikia ombi hilo na itatoa jawabu hivi karibuni
No comments:
Post a Comment