VETA NA UJERUMANI WATILIANA SAINI MAKUBALIANO YA MAFUNZO YA UWANAGENZI KATIKA TEKNOLOJIA YA UFUNDI WA ZANA ZA KILIMO NA MITAMBO YA UJENZI
Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetiliana saini makubaliano yenye thamani ya Euro 900,000 (zaidi ya shilingi bilioni 2.3) na Chemba ya Baraza la Ufundi Stadi ya Ujerumani (WHKT) kwa ajili ya mafunzo ya uwanagenzi yenye lengo la kuimarisha ufundi wa zana za kilimo na teknolojia ya mitambo ya ujenzi.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Moshi Kabengwe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Leonard Akwilapo na Ujerumani aliyetia saini ni ni Mtendaji Mkuu wa Ujerumani , Reiner Nolte na kushuhudiwa na Barozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter, Mwenyekiti wa Board ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,Peter Maduki, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dk. Bwire Ndazi na Maafisa wengine waandamizi wengine wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, VETA na Ujerumani.
“ujuzi wa mafundi na wakulima utaboreshwa kupitia kozi zitakazotolewa na VETA kwa mfumo wa uwanagenzi. Kozi hizo ni pamoja ufundi zana za kilimo, ufundi mitambo ya ujenzi na mafunzo ya vitendo katika teknolojia ya kupunguza upotevu wa mavuno ya mazao ya kilimo katika maeneo yatakayoainishwa,” inaeleza sehemu ya waraka wa makubaliano.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Balozi wa Ujerumani nchini Dk. Detlef Waechter alisema anatarajia kuwa ushirikiano katika mradi huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wengi, hususani vijana katika kupata ujuzi wa kuutumia kwenye kuongeza tija kwenye kilimo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimani watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Moshi Kabengwe aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa msaada na ushirikiano na kusema kuwa utawasaidia vijana wengi kuajirika na kuwa na ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire Ndazi aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuiamini VETA na kuendeleza ushirikiano nayo katika utoaji mafunzo kwa mfumo wa uwanagenzi. Amesema, ushirikiano katika miradi ya nyuma umeendelea kuwanufaisha vijana wengi kupata ujuzi na kuweza kuajirika kwa urahisi.
Mafunzo ya uwanagenzi uendeshwa kwa mfumo wa ngwe za mzunguko kati ya chuo cha ufundi stadi na sehemu ya kazi ambapo mwanafunzi hupata mafunzo ya ujuzi kwenye karakana za chuo na uzoefu wa hali halisi mahala pa kazi, hivyo kumwongezea umahiri pamoja na maarifa zaidi na utamaduni wa ya mazingira ya kazi husika.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Moshi Kabengwe akisaini makubaliano ya uendelezaji wa mafunzo ya uwanagenzi kulia ni ni Mtendaji Mkuu wa Ujerumani , Reiner Nolte na wanaoshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire na Balozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire Ndazi akizungumza katika mkutano wa kutiliana saini ya makubaliano kati ya Ujerumani na VETA kwa ajili mafunzo ya uwanagenzi yenye lengo la kuimarisha ufundi wa zana za kilimo na teknolojia ya mitambo ya ujenzi.
Picha ya Pamoja Balozi wa Dk. Detlef Waechter akipeana mkono Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimani watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji, Moshi Kabengwe pamoja na watendaji wa VETA Wawakilishi Ujerumani baada ya kusaini makubaliano ya kuendeleza wanagezi.
No comments:
Post a Comment