Na Pamela Mollel-Arusha
WAZIRI wa Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Jenista Mhagama
amezitaka hifadhi za taifa nchini kuendelea kuwatumia wasanii nchini
katika kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana huku akiipongeza
Mamlaka ya hifadhi za taifa Ngorongoro inavyotangaza vivutio vyake
kupitia msanii Mrisho Mpoto.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni jijini Arusha alipotembelea banda la Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro katika maonesho ya Nanenane.
Alisema kuwa wasanii wananafasi kubwa ya kuutangaza utalii wa ndani na
kuendelea kuitangaza Tanzania endapo watatumiwa kama mabalozi kupitia
umaarufu wao jambo ambalo litasaidia pia kuiingizia nchi kipato kupitia
watalii.
Naye Balozi wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Mrisho Mpoto aliwapongeza watanzania kuwa na mwitikio mkubwa wa kutembelea hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto wao katika maonesho hayo ili kujifunza na kuona shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo hivyo kuwaandaa watoto hao kuwa wahifadhi kwa baadae.
“Mfano mzuri ni hili la punguzo la shilingi elfu 50 lililotolewa ili
watanzania waweze kutembelea hifadhi ya Ngorongoro tumeona watu
walivyochangamkia na kwenda kutembelea Ngorongoro hivyo ni jambo zuri
na la kupongezwa kwa watanzania na ninaomba waendelee kutembelea
hifadhi zetu”alisema Mpoto.
Kwa upande wake Ofisa Utalii wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Peter
Makutian aliwashukuru watanzania kuendelea kuhamasika kutembelea hifadhi hiyo tofauti na awali na kusema kuwa idadi ya wageni toka nje ya nchi wanaotembelea hifadhi hiyo kwasasa ipo sawa na watanzania.
Aidha aliwaomba watanzania wengine kuendelea kutembelea vivutio vya Tanzania ikiwemo Ngorongoro kwakuwa gharama wanazotoza ni ndogo kwao ukilinganisha na wageni toka nje ya nchi hivyo ni fursa nzuri kwao
kuitumia na kuwa mabalozi wa hifadhi kwa wengine.
WAZIRI wa Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Jenista Mhagama akiwa anamsikiliza Balozi wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Mrisho Mpoto mara baada ya kuwasili katika banda hilo hivi karibuni jijini Arusha katika maadhimisho ya sikukuu ya nane nane
Ofisa Utalii wa Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro Peter Makutian aliwashukuru watanzania kuendelea kuhamasika kutembelea hifadhi hiyo tofauti na awali na kusema kuwa idadi ya wageni toka nje ya nchi wanaotembelea hifadhi hiyo kwasasa ipo sawa
na watanzania.
No comments:
Post a Comment