Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido, kulia kwake ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo na kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Longido Bw. Daniel Chongolo.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo amewashukuru na kuwapongeza wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamejitoa na kuhakikisha wanakamilisha jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido.
Akizindua jengo hilo jana, alisema kwamba litawezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa utulivu sambamba na kukabiliana vyema na masuala ya uhalifu katika wilaya hiyo, na kuongeza kuwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa anajisikia furaha na fahari kuona wadau wanashirikiana na kuagiza meneja wa Tanesco wilaya ahakikishe ameweka mita ya umeme ambapo gharama hizo aliahidi atazitoa yeye mwenyewe.
“Lazima tuimarishe mipaka na Polisi wawe na vituo vya uhakika vya kufanyia kazi ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhalifu na Jeshi hilo litaendelea kutumia mbinu shirikishi”. Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Bw. Gambo aliwaasa baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji pamoja na wananchi kutoficha wageni ambao wanaishi nchini bila kufuata sheria na kuongeza kuwa yeyote atakayegundulika anafanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
“Kila kiongozi anapaswa kutambua watu wote wanaoishi katika eneo lake na kuhakikisha mgeni yoyote amefuata sheria na kama akigundua (Anaishi bila utaratibu) atoe taarifa kupitia kamati za ulinzi na usalama za kata ili hatua ziweze kuchukuliwa”. Alisisitiza Bw. Gambo.
Akizungumza katika uzinduzi huo mwenyeji wa shughuli hiyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Omari Mkumbo mbali na kuwashukuru wadau hao, alisema kwamba tukio la uchangiaji na ukamilishaji wa jengo hilo limeonyesha kwamba wana Longido wana mshikamo wa hali juu.
Kamanda Mkumbo alisema kwamba wananchi waendeleze mshikamo huo ili kuweza kuimarisha kituo kingine cha Polisi kilichopo tarafa ya Kamwanga na kutaja majengo mengine ambayo yanajengwa na kukaribia kukamilika kwa hamasa ya Mkuu wa mkoa kuwa ni kituo cha Polisi cha Kwa Morombo pamoja na kituo cha Polisi cha Utalii ambacho ujenzi wake unafadhiliwa na TATO (Tanzania Tourist Operators).
“Kazi kubwa ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na japokuwa takwimu za matukio ya uhalifu katika wilaya hiyo yapo chini lakini bado kuna tatizo la madawa ya kulevya aina ya Bhangi na Mirungi hivyo wananchi endeleeni kutoa ushirikiano kwa askari kwani madhara ya madawa hayo ni makubwa”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo alisema ongezeko la ukamataji wa madawa ya kulevya umetokana na udhibiti mzuri na kuahidi kuimarisha zaidi usalama kwa kutumia Polisi na vyombo vingine vya usalama huku akitoa shukrani zake kwa Kamanda wa Polisi mkoa kwa kutoa gari ambalo litasaidia kuimarisha ulinzi katika tarafa ya Kamwanga.
Awali akitoa taarifa ya uhalifu pamoja na mchakato wa ujenzi huo, Mkuu wa Polisi wilaya ya Longido Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Joswam Israel Kaijanante alisema kwamba ujenzi huo umegharimu zaidi ya Milioni 80 ambazo zilichangwa na viongozi, askari pamoja na wananchi na kuongeza kwamba bado jengo hilo halina samani na “Kompyuta , Printer” pamoja na mfumo wa maji taka ambapo gharama zake ni Milioni 16.
Mchakato wa ujenzi wa jengo hilo ambao una ofisi tatu ambazo ni za Mkuu wa Polisi wilaya, Mkuu wa Upelelezi wilaya na Mwendesha Mashtaka wa Polisi ulianza mwaka 2015 na kukamilika mwezi Julai mwaka huu uliwashirikisha kikamilifu jumla ya wadau wapatao 20 ambao pia walipewa vyeti vya shukrani.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wakati akifungua jiwe la msingi lililowekwa katika ujenzi wa jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido.
Jengo jipya la utawala Polisi wilaya ya Longido ambalo lilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo jana katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
No comments:
Post a Comment