Wananchi 365 wa kijiji cha Chongoleani watafidiwa shilingi bilioni 3,035 kwa ajili ya kutoa maeneo yao, ili kupisha ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga.
Hayo yamesemwa na Meneja Mawasiliano wa Shirika la Usimamizi wa Bandari Tanzania TPATanga, Bibi Janeth Rwuzangi katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO) leo.
Bi Ruzangi amesema kuwa kwa hapa Chongoleani mradi una ukubwa wa hekta 200 zikiwemo hekta 100 zitakazotumiwa kuweka miundombinu ya mafuta ghafi. Hekta 100 zilizosalia zitatumika kwa ajili ya shughuli za TPA) kuwekeza miundombinu ya kupokea mafuta yaliyosafishwa. Vile vile eneo hili limezingatia maendeleo endelevu ya biashara ya mafuta na gesi katika siku zijazo.
Aliongeza kuwa TPA itakuwa na wajibu wa kuhudumia meli, kuhakikisha usalama wa bidhaa, vyombo na watu pamoja na kusimamia masuala ya afya bandarini. Aidha, Majukumu la TPA yanatarijiwakujikita katika shughuli za uendeshaji wa majini ikiwemo kuwa na vyombo na boti maalumu kwa ajili ya kuongozea meli wakati wa kuingia na kutoka kwenye gati la mafuta ghafi.
Akitoa ufafanuzi, Bi Ruzangi amesema vile vile, TPA ina jukumu la kuhakikisha inahudumia shehena ya vifaa vyote vya ujenzi katika Bandari ya Tanga kwa kushirikiana na Bandari Kuu ya Dar es Salaam. Shughuli nyingine ni pamoja na ulinzi wa miundombinu ya majini pamoja na usalama wa eneo la Bandari ambalo limegawanyika katika sehemu kuu mbili; ardhini kwenye gati la mafuta na majini kwenye lango la kuingilia meli na nangani.
Kwa upande wa ajira za TPA Ruzangi amesemawafanyakazi ambao wataajiriwa ni pamoja na mabaharia, wahandisi, mafundi, wahasibu, wachumi, watakwimu, vibarua mbalimbali kwa ajili ya nguvu kazi n.k. Sehemu ya wafanyakazi hawa watatokana na waliopo sasa kwenye Bandari watakaopangiwa kazi hizo. Hata hivyo TPA inatarajia kuajiri wengine ambao watalazimika kufanya kazi hizo kulingana na taratibu za ajira za TPA.
Pamoja na kuwa na bomba la mafuta, kijiji cha Chongoleani kitafaidika na ujenzi wa barabara ya kilometa 8 itakayounganisha bandari na barabara kuu ya Horohoro – Tanga, ambapo kwa kiasi kikubwa itainua uchumi wa wananchi wanaoishi maeneo hayo kusafirisha mazao, samaki na bidhaa nyingine kwa urahisi.
Akifafanua uwekaji wa jiwe la msingi Ruzangi amesemakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli na Mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wanatarajia kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta tarehe 05 Agosti 2017.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Chongoleani, Bw. Mbwana Nondo amesema; “Kwa moyo wa dhati kabisa, naomba nimshukuru sana sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kwa kutujali wananchi wake na kutuletea neema ya Mradi wa Bomba la Mafuta, katika maisha yetu wanachongoleani, hatutaweza kumsahau kwa kizazi hiki kinachoshuhudia mradi huu na vizazi vijavyo”.
Nondo alisema kuwa anamuhakikishia Mhe. Rais kuwa kuwa wote watakaopata fursa kwenye mradi wa Bomba la Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Bomba la Mafuta la kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga Chongoleani lina urefu wa Kilometa 1445 ambapo kwa upande wa Tanzania itakuwa na jumla ya kilometa 1115 na Uganda 330. Aidha, Mradi utatarajia kusafirisha mapipa laki mbili na kumi na sita elfu (216,000) kwa siku .
Kijiji cha Chongoleani ndio kituo cha mwisho ambapo mitambo mikubwa itasimikwa katika eneo hili kwa ajili ya kusukuma mafuta eneo la baharini ili, kuweka kwenye vyombo vya usafirishaji kusafirisha maeneo mbalimbali duniani ambayo Uganda watakuwa wamepata soko.
Tanzania itafaidika na mradi huu kutokana na kodi, tozo na mrahaba wa bomba la mafuta, itakayofanywa moja kwa moja na mradi huo. Faida nyingine ambazo, sio za moja kwa moja ni ajira, fursa za kufanya biashara na uwezekano wa mikoa 8 ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na Tanga.
No comments:
Post a Comment