Thursday, August 31

Waislamu milioni mbili waanza ibada ya Hajj Mecca

Mecca Hajj (30 Agosti 2017)Haki miliki ya pichaAFP
Image captionMahujaji zaidi ya 1.7 milioni kutoka nchi mbalimbali wamesafiri kwenda Mecca kwa Hajj
Mahujaji karibu milioni mbili kutoka nchi mbalimbali duniani wameanza kuwasili Saudi Arabia kwa ibada ya Hajj ambayo hufanyika kila mwaka.
Walianza machweo Jumatano kwa kuzunguka Kaaba katika Msikiti Mkuu wa Mecca, eneo takatifu zaidi katika dini ya Kiislamu.
Raia wa Iran kwa mara nyingine wanashiriki baada ya kukosa Hajj ya mwaka mmoja kutokana na mkanyagano uliotokea mwaka 2015.
Kulikuwa na taarifa za kukinzana kuhusu idadi kamili ya mahujaji wanaohudhuria kutoka taifa jirani la Qatar, ambalo limekuwa kwenye mzozo mkali na Saudi Arabia.
Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu, ambayo inafadhiliwa na serikali ya Qatar, imesema ni raia wachache sana wa Qatar ambao wamevuka mpaka, ambao ulifunguliwa wiki mbili zilizopita na serikali ya Saudia kuwawezesha Waislamu kuhiji.
Lakini gavana wa Mecca amesema raia 1,564 wa Qatar wanashiriki ibada hiyo ya Hajj, idadi ambayo imeongezeka ukilinganisha na 1,210 mwaka jana.
Kwa Waislamu, Hajj ndiyo nguzo ya tano na ya mwisho ya dini ya Kiislamu.
Ni ibada ambayo Mwislamu yeyote aliyekomaa anashauriwa kutimiza angalau mara moja maishani mwake iwapo anaweza kulipia gharama na ana nguvu za kimwili kuweza kutimiza abada hiyo.
Mahujaji pia hupanda Mlima Arafat, 20km (maili 12) mashariki mwa MeccaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMahujaji wakipanda Mlima Arafat, 20km (maili 12) mashariki mwa Mecca Jumatano
Serikali ya Saudia imesema imechukua tahadhari kuzuia kutokea tena kwa mkanyagano sawa na uliotokea miaka miwili iliyopita.
Maafisa wa Saudia wanasema mahujaji karibu 800 walifariki wakati wa mkanyagano huo, lakini takwimu zisizo rasmi zinasema watu zaidi ya 2,400 walifariki.
Iran pekee ilikuwa na raia 464 waliofariki na baada ya hapo iliwatuhumu maafisa wa Saudia ikisema wanafaa kulaumiwa kwa vifo vilivyotokea.
Maafisa wa Saudia walikanusha tuhuma hizo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa Saudia Meja Jenerali Mansour al-Turki amesema maafisa wa usalama zaidi ya 100,000 wametumwa katika maeneo mbalimbali ya Mecca na Medina kulinda na kuwaelekeza mahujaji.
Aidha, kuna kamera nyingi sana za usalama.

No comments:

Post a Comment