31/08/2017 Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa kujituma, kuongeza ufanisi na kutoa huduma bora kwa wagonjwa ili epukana na malalamiko yanayoweza kujitokeza.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof. Janabi pia aliwahimiza wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuendelea kutunza vizuri kumbukumbu mbalimbali zikiwemo za wagonjwa na utendaji wa kazi zao za kila siku ili pale zitakapohitajika zipatikane kwa haraka.
“Mjitahidi kujaza fomu ya wazi ya mapitio na upimaji utendaji kazi (OPRAS) kwa wakati ili kusiwe na malalamiko ya upandaji wa vyeo kwani ujazaji wa fomu hizo ndiyo unaowezesha mfanyakazi kupimwa utendaji wake kwa kipindi cha mwaka mzima”, alihimiza Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Godfrey Tamba aliupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi zao katika mazingira bora.
Tamba alisisitiza, “Wafanyakazi wenzangu tunaodai haki zetu tukumbuke kutimiza wajibu wetu wa kazi kwa wakati, kwani uongozi wa TUGHE hautawatetea watu ambao hawatimizi wajibu wao ipasavyo”.
Hiki ni kikao cha pili cha wafanyakazi wote kufanyika tangu kuanza kwa mwaka huu ambapo katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
No comments:
Post a Comment