Tuesday, August 15

Viongozi, wanachama 51 wa Chadema waanza kutoka kwa mafungu


Chato. Viongozi na wanachama wa Chadema 51 waliokuwa wakisota rumande wakidaiwa kufanya mkusanyiko bila kibali Julai 7, wameanza kupata dhamana kwa mafungu baada ya polisi kupeleka gari Gereza la Biharamulo lililowafikisha kituo cha polisi cha Chato.
Viongozi na wanachama hao waliopata dhamana tangu Julai 26 waliendelea kukaa rumande baada ya polisi kusema hawakuwa na gari la kuwafikisha mahakamani kukamilisha taratibu.
Fungu la kwanza la watu 14 lilifikishwa mahabusu ya kituo cha polisi Chato kusubiri wadhamini wao wanaotarajiwa kufika mahakamani leo kukamilisha taratibu za dhamana.
Katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Rehema James alisema washtakiwa hao walifikishwa wachache licha ya gari walilopewa kuwa na uwezo wa kubeba washtakiwa 40.
“Tumeelezwa wapo washtakiwa wengine wanaohitaji kuletwa mahakamani wapate dhamana na wapo zaidi ya mwezi mzima hivyo hawawezi kuleta wa Chadema pekee kwa kuwa mahitaji ni mengi na wengi hawafikishwi mahakamani kutokana na kukosa gari,” alisema Rehema
Alisema polisi wamewaelekeza kuwa gari hilo litaendelea kufanya kazi ya kuwaleta watu mahakamani kwa wiki nzima lakini si kwa ajili ya washtakiwa wa Chadema hivyo kutojua hatma ya waliobaki watatoka lini.
Miongoni mwa waliotoka ni wanawake sita na wanaume saba ambao ni wanachama na kiongozi mmoja Mange Sayi, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Chato.
Viongozi na wafuasi 51 wa Chadema walikamatwa Julai 7 kwenye Ukumbi wa Manzagata Kata ya Muganza wilayani Chato wakiwa kwenye kikao cha ndani na kushtakiwa kwa kosa la kufanya mkusanyiko bila kibali.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Chato, Jovis Kato aliwaachia kwa dhamana Julai 26, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kati ya mashitaka na washitakiwa huku upande wa mashitaka ukiomba mahakama iwanyime dhamana washtakiwa hao ili waendelee na upelelezi.
Kato alisema baada ya kuzipitia hoja zote kwa kina, mahakama imekubali ombi la upande wa utetezi kuwa kifungu namba 148(5) kilichowekwa na upande wa mashtaka cha kuzuia dhamana za washitakiwa hakiendani na zuio hilo. Alisema kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 13(6)(b) inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshitakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.
Aliweka dhamana za washtakiwa hao 51 wazi tangu Julai 26 ambazo walitimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh500,000 kila mmoja lakini hadi sasa bado wapo magereza.

No comments:

Post a Comment