Tuesday, August 15

anzania yalenga makubwa Misri

Rais John Magufuli akisalimiana na mgeni wake,

Rais John Magufuli akisalimiana na mgeni wake, Abdel Fattah el-Sisi wa Misri Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu. 
Dar es Salaam. Tanzania ina malengo ya kimkakati ya kuboresha uhusiano wake na Misri, Rais John Magufuli alisema jana mbele ya mgeni wake, Rais Abdel Fattah El-Sisi jijini Dar es Salaam jana.
Viongozi hao wawili walikubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii baada ya kiongozi huyo wa taifa la Kiarabu kufanya mazungumzo na Rais Magufuli jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais John Magufuli aliwaambia wanahabari kuwa wamekubaliana na El-Sisi kukuza biashara kwa Serikali ya Misri kuanzisha kiwanda cha nyama hapa nchini.
“Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi na Misri wana shida na nyama. Kiwanda kikianzishwa hapa nyama zitakuwa zinasafarishwa kutoka Tanzania hadi Misri na nchi nyingine,” alisema Rais Magufuli.
“Hatua hii itasaidia Serikali kupata mapato sanjari na wafugaji kupata soko la mifugo yao.”
Mbali na hilo, Rais Magufuli alisema wamekubaliana na mgeni wake kuwa Misri isaidie Tanzania katika sekta ya afya, akisema nchi hiyo itatoa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema hatua hiyo itasaidia Muhimbili kutoa huduma ya operesheni ya figo na masuala mengine.
Pia alisema Serikali ya Misri ipo tayari kuisadia Tanzania katika teknolojia ya umwagiliaji kwa kuwa wapo juu katika suala hilo.
Kuhusu utalii, Rais Magufuli alisema Misri ipo tayari pia kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya utalii pamoja na mashirika ya usafiri wa anga ya nchi hizi mbili.
“Tanzania ukimjulisha na Zanzibar tunapata watalii wasiozidi milioni mbili kwa mwaka. Wakati wenzetu wanapata milioni kumi. Kwa hiyo tutabadilishana ili watusaidie katika jambo hili ili tuongeze idadi ya utalii,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kupitia uhusiano ulipo kati ya Tanzania na Misri, hivi sasa kuna Watanzania 115 wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini humo na kwamba serikali hiyo imeamua kuongeza idadi ya wanafunzi katika programu tofauti.
“Tutakuwa tukibadilisha walimu katika programu mbalimbali na nipo tayari kutoa walimu wa Kiswahili ili waende kufundisha vyuo vikuu vya Misri na wao wamesema watatoa wataalamu wa teknolojia na habari (IT) na walimu wa lugha ya kiarabu watakaofundisha hapa nchini,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kumshukuru rais huyo wa Misri na kwa upendo alionao kwa Watanzania na kwamba wamejifunza mambo mengi kutoka Misri na wanaithamini ziara yake.
Alisema rais wa Misri ni mwanajeshi aliyefikia cheo cha Field Marshal ambaye anataka kazi ifanyike, kitu ambacho kinaendana na falsafa yake ya “hapa kazi tu”, hivyo kuwataka mawaziri wa nchi hizo mbili kujipanga ipasavyo kuendana kasi hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais El-Sisi alisisitiza umuhimu wa kukuza biashara hasa katika sekta ya madini na madawa.
Alisema uhusiano baina ya mataifa hayo utaimarishwa zaidi na biashara.
Alisema nchi yake itaongeza uwekezaji hapa nchini katika sekta za ujenzi, uhandisi na miundombinu. Pia aliongeza kuwa nchi hizo zitaongeza ushirikiano katika kubadilishana wataalamu katika nyanja mbalimbali.
Kuhusu suala la amani, Rais El-Sisi alisema nchi yake itaendelea kushirikiana kwa ajili ya amani ya bara la Afrika na maendeleo ya bara hili.
“Napongeza jitihada za Tanzania katika kuleta amani eneo la maziwa makuu ikiwa ni jitihada za (Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa, pia kupokea wakimbizi katika ukanda huu,” alisema El-Sisi.
El-Sisi alimpongeza Rais Magufuli kwa kupambana na ufisadi na kuwekeza kwenye maendeleo na kusema kwamba ziara yake itarudisha uhusiano baina ya Tanzania na Misri.

No comments:

Post a Comment