Upinzani nchini Kenya umeishutumu serikali kwa kutekeleza 'ugaidi' dhidi ya raia wake na kuapa kubadilisha matokeo ya uchaguzi mkuu walioyataja kuwa ya 'uwongo'.
Afisa mwandamizi katika upinzani huo James Orengo amesisitiza kuwa hawatakwenda mahakamani ili kuafikia lengo lao.
Amewataka wafuasi wao kuwa watulivu na kujilinda dhidi ya 'madhara' ya serikali.
Bwana Orengo amedai kwamba takriban watu 100 ikiwemo watoto wameuawa na vikosi vya usalama vya Kenya huku miili yao ikitiwa ndani ya mifuko ya plastiki.
Alionyesha vibweta vya risasi lakini akashindwa kutoa ushahidi kuthibitisha madai hayo.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa rais Uhuru kenyatta alipata asilimia 54.3 ya kura huku mpinzani wake mkuu Raila Odinga akitaja matokeo hayo kama ''mchezo mkubwa''.
''Walijua kwamba wataiba kura .Walijua kwamba watu hawatafurahia kwa hivyo vifaa vyote vya kukabiliana na ghasia viliwekwa tayari'', alisema Orengo.
Huku ikiwa waandishi hawajaona ushahidi wa kuthibitisha mauaji hayo yanayodaiwa na upinzani, takriban watu 11 wameripotiwa kuuawa na polisi katika maeneo yanayomuunga mkono Raila Odinga.
Chumba cha kuhifadhi maiti cha kaunti ya Nairobi kilipokea miili minane.
Watu wengine watatu waliripotiwa kuuawa katika kisa chengine, ikiwemo mtoto wa miaka tisa aliyepigwa na risasi kwa bahati mbaya katika mtaa wa mabanda wa Mathare uliopo Jiji Nairobi.
Mtu moja pia aliuawa mjini Kisumu , ambayo ni ngome ya upinzani na eneo la ghasia za kikabilia wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, wakati ambapo takriban watu 1200 walifariki na wengine 600,000 kuachwa bila makao.
Mapema shirika la wangalizi wa uchaguzi ELOG ambalo lilikuwa na waangalizi 8,300 lilisema kuwa matokeo yake yalimpatia rais Kenyatta asilimia 54 ya kura hizo.
Lakini Bwana Orengo amekosoa uhuru wa shirika hilo.
Awali kaimu waziri wa usalama wa ndani nchini k
Kenya Fred Matiangi aliwataka Wakenya kurudi katika maisha yao ya kawaida na kuwataka wale wanaotumia mitandao ya kijamii kuitumia vizuri.
Rais Kenyatta ameomba kuwepo na amani.
''Tumeona matokeo ya ghasia za baada ya uchaguzi , Najua kwamba hakuna Mkenya mwengine ambaye angependa kurudi katika ghasia hizo'', alisema.
Kabla ya matokeo hayo kutangazwa bwana Raila Odinga aliwaomba wafuasi wake kuwa watulivu, lakini akongezea kuwa hawezi kumdhibiti mtu yeyote na kwamba watu wanataka kuona haki.
Shirika la haki za kibinaadamu la Amnesty International limeitaka serikali kuchunguza mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment