Friday, August 18

Uamuzi pingamizi kesi ya Wema kutolewa Agosti 31


Dar es Salaam. Uamuzi wa kupokea au kutopokea   kielelezo cha ushahidi cha msokoto mmoja wa bangi na vipisi viwili vya bangi katika kesi inayomkabili mlimbwende wa Tanzania 2006, Wema Sepetu utatolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwisho wa mwezi huu.
Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba amesema uamuzi huo ulipaswa autoe leo, lakini bado kuna tafiti anazifanya, hajakamilisha hivyo aliuahirisha hadi Agosti 31,2017.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka ataendelea kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Septemba 12 na 13, 2017.
Uamuzi huo umefuatia baada ya shahidi huyo ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima ambaye alipima msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua ni bangi, kuomba kuvitoa mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi.
 Mulima kupitia wakili wa Serikali, Costantine Kakula aliomba kuitoa bahasha iliyofungwa juu yenye muhuri, saini ya shahidi huyo na namba ya maabara 291 ya 2017  ambayo ndani yake kulikuwa na msokoto na vipisi viwili vya bangi mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi.
Hata hivyo wakili wa Wema, Tundu Lissu alipinga kisipokewe kama kielelezo cha ushahidi kwa sababu ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Simba alisema Agosti 18, 2017 atatoa uamuzi juu ya hoja hizo na kesi hiyo pia inaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

No comments:

Post a Comment