Monday, August 21

TFS KUPANDA MITI KATIKA HEKTA LAKI 182 KILA MWAKA, KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MISITU NCHINI


Na  Tiganya Vincent - TABORA

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imepanga kupanda miti katika hekta 182,000 kwa mwaka ili kukabiliana na uharibifu wa misitu uliotokana na shughuli mbalimbali za binadamu hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana na Afisa Misitu na Mtalaalamu, Mshauri wa Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu wa TFS, Dkt. Ismail Aloo wakati akiongea kwenye kikao cha utekelezaji wa randama ya ushirikiano wa usimamizi wa rasilimali za misitu kanda ya magharibi.

Alisema kuwa hali ya uharibifu wa misitu hapa nchini inatisha ambapo hekta 372,000 kila mwaka zinaharibiwa kutokana na kilimo cha kuhama hama , uchomaji mkaa, mifugo isiyozingatia ufugaji bora na uchanaji mbao usiozingatia taratibu na sheria. Dkt. Aloo aliongeza kuwa  ili kukabiliana na tatizo hilo juhudi zaidi zinahitajika katika upandaji miti kwa ajili ya kuziba pengo la uharibifu wa mistu ambao  umeifanya Tanzania kuwa  uhaba miti kwa ujazo wa mita wa miti milioni 19.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo alisema kuwa ni marufuku kwa viongozi wa vijiji kuwaagiza wananchi kufyeka misitu katika maeneo wanayomiliki kwa kisingizio cha uendelezaji wa sehemu zao. Alisema kuwa viongozi hao lazima watambue kuwa misitu ya hapa nchini ina thamani ni lazima wahakikishe wanaitunza kwa kusimamia sera na sheria na sio wao kuwa chanzo cha uharibifu.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwaagiza Wakuu wa Wilaya mkoani Tabora kushirikiana na Watendaji wa TFS katika kuhakikisha wanasimamia Sera na Sheria katika kuwaondoa watu wote waliovamia mistu ya hifadhi. Alisema kuwa suala la kusimamia mistu na kuifanya iwe endelevu haliwezi kuwa TFS pekee bali linahitaji nguvu za pamoja ikiwemo kutoka katika Halmashauri husika. Bw. Mwanri alisema kuwa uharibifu ukiendelea katika mistu haitalaumiwa TFS pekee bali hata viongozi wengine katika maeneo husika watabeba lawama hizo.

“Kama tutashirikiana  fahamu kuwa hakuna jambo ambalo litatushinda katika kukabiliana na watu wanaoharibu mistu na kutishia maisha ya wananchi” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwaagiza Watendaji mbalimbali kuanza kuelimisha wananchi umuhimu wa matumizi ya majiko sanifu yanayotumia mkaa kidogo ili kupunguza mahitaji ya nishati hiyo ambayo nayo ni miongoni mwa matishio ya mistu.

No comments:

Post a Comment