Ukikutana na hali hiyo fuatilia kwa karibu kufahamu huwa wanatizama nini, mbali na hiyo kuwa makini pia na katuni, kwa sababu zipo zisizofaa.
Inawezekana walikuwa wanaangalia picha za ngono. Usiache kufuatilia kwa sababu wana umri wa miaka mitano, tafiti mbalimbali zinaonyesha wapo watoto wenye umri usiozidi miaka sita na tayari wametizama picha hizo mara kadhaa.
Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Nebraska-Lincoln nchini Marekani, wametafiti tabia ya watoto hususani wa kiume wanaotizama picha hizo wanapokuwa wakubwa.
Utafiti umeangalia uhusiano kati ya kuangalia picha katika umri mdogo na matendo ya uhusiano wa mapenzi baadaye.
Umebaini vijana wa kiume wanaoangalia wakiwa wadogo huwa hawana utaratibu mzuri katika mapenzi na huwachukulia wanawake kama chombo cha kutimiza matakwa yao.
Utafiti huo pia ulibaini vijana hao huwa na tabia ya kutaka kushiriki tendo la ndoa kwa kutumia nguvu na aina mbalimbali za mitindo.
Wamepata uhusiano wa kati ya umri ambapo mvulana anayetizama picha hizo chafu huwa na mtizamo wa ubaguzi wa kijinsia baadaye hususani wa kingono.
“Hujiona wanafahamu kila kitu kuhusu mapenzi, ikiwamo kuwa na asilimia kubwa ya tabia za kupenda kutumia nguvu na namna za kuudhi na kukera wakiwa faragha, ” anasema Dk Bischmann.
Akiuzungumzia utafiti huo mpya uliochapishwa Agosti 3 mwaka huu kwenye tovuti ya Dailymail, Dk Alyssa Bischmann mhadhiri wa chuo kikuu hicho alisema lengo la utafiti lilikuwa ni kufahamu madhara ya awali anayopata kijana anayetizama picha za ngono akiwa na umri mdogo.
Anasema walilenga zaidi kanuni mbili za kufanya ngono ambazo ni kupenda sana tendo hilo au kuwatumia wanawake kwa nguvu anaposhiriki tendo hilo na kutamani wafanye zaidi ya wanachokifanya.
Bischmann na wenzake waliwafanyia utafiti wanaume 330 wenye umri kati ya miaka 18 na 54 katika Chuo Kikuu cha Mid Western, ambacho pia huwa na wataalamu wa afya.
Anasema kila mtu aliulizwa juu ya kujihusisha kwake kwa mara ya kwanza kuangalia picha hizo alikuwa na umri gani na ilikuwa ni kwa makusudi, bahati mbaya au kwa kulazimishwa.
Washiriki waliulizwa mfululizo wa maswali 46 ili kupima uelewa wao na utendaji katika kanuni mbili za kujamiiana na matendo yao ya ukatili dhidi ya wanawake kingono.
Anaeleza asilimia 43.5 walisema waliona picha hizo kama ajali, asilimia 33.4 walisema walitizama kwa hiyari yao na asilimia 17.2 walisema walilazimishwa huku asilimia sita wakikosa jibu.
“Tumegundua vijana wengi walioanza kuona picha hizo mapema wamekuwa na tabia za kutumia nguvu katika mapenzi na kutaka kuona aina na mitindo tofauti, ukilinganisha na walioangalia picha hizo ukubwani, ” anasema Dk.
Dk anafafanua kuwa jibu hilo wamelipata kwa kufuata mtiririko wa mahojiano ya vijana wadogo wa miaka mitano na wakubwa wa miaka 26, ambao kwa pamoja majibu yao yalifanana.
Anataja miongoni mwa majibu yao ni kutotaka kukutana kimwili na wanawake kawaida bila kuonyesha kuwa wao wanaweza.
“Nataka hadi alie, abadilike rangi, avimbe na ikiwezekana siku ya kwanza anichukie kabisa, ” alisema mmoja wa vijana waliohojiwa.
Anasema utafiti huo pia ulibaini mwanaume mtu mzima akitizama picha za ngono kwa mara ya kwanza hutamani kufanya mapenzi na wanawake wengi na kurudi katika umri mdogo.
Mwandishi mwenza wa utafiti huo Chrissy Richardson, anasema hawakutegemea kupata matokeo hayo.
Anasema walichobaini hawakukitegemea kwa sababu walidhani kutizama picha hizo hakutakuwa na athari hasa kwa watoto wadogo, lakini imekuwa kinyume ambapo wamekuwa na athari kuliko wanaume wakubwa.
Anasema hawakudhani kama kuangalia picha hizo kungekuwa na athari katika ushiriki wa ngono halisia.
Watalaamu wanena
Mtaalamu wa saikolojia Dk Theopista Rutayunga anasema kuwa kisaikolojia wanaume wamezaliwa viongozi, hivyo kadri wanavyokuwa wanataka utawala hususani kwa wenza wao.
Anasema hata akiwa na hekima kiasi gani, mpole na msikivu hali ya kuwa mtawala haiondoki, tofauti itakuwa ni jinsi anavyowasilisha utawala wake.
“Kuhusu kuangalia picha za ngono sijafanya utafiti na kupinga au kukubaliana na hao waliofanya, lakini nakubaliana nao kuwa wanaume wanapenda kuwa watawala hususani wanapokuwa na wenzi wao, ” anasema Dk Rutayunga.
Dk Rutayunga anasema watoto ni rahisi kunakili kichwani kitu wanachokiona au kukisikia, ndiyo maana wazazi wanashauri kuwa makini hata katika mazungumzo ya kawaida.
“Kisaikolojia watoto hawana vitu vingi kichwani, hivyo kila kinachopita karibu yao kinaingia kichwani moja kwa moja, mara nyingi akili hupenda kile kinachokatazwa badala ya kinachohimizwa, hivyo inawezekana utafiti wao una ukweli kwa maantiki hiyo.
Naye mtaalamu wa saikolojia Modester Kamongi anasema siyo tu watoto wa kiume, mtoto yoyote akiona jambo katika umri mdogo linamkaa kichwani na kuamini kuwa hayo ndiyo maisha.
Anasema kwa wanaume kutaka kutawala jambo lolote wanalofanya na wenza wao hayo ni maumbile na taratibu zilizopo.
“Unajua saikolojia za wanaume wengi zimeathiriwa na mila na tamaduni, watoto wa kiume wamekuwa wakichukuliwa kama ndiyo ngao kwenye familia, kuanzia urithi, kufanya maamuzi, kusoma na wanapooa pia husisitiziwa jambo hilo, ” anasema Kamongi.
Kamongi anaeleza sababu zote hizo na nyingine nyingi tayari zinampa mwanaume nafasi kubwa kuwa mtawala wa mwenza wake.
“Siwezi kusema sana kuhusu huo utafiti, lakini ninachofahamu mwanaume hawezi kukubali mwanamke amshinde hata kama jambo haliwezi atajitutumua na akishindwa atalipiga vita, ndiyo saikolojia yao ilivyo, ” anasema.
No comments:
Post a Comment