Kaya hizo ni miongoni mwa zilizowekewa alama ya X na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa lengo la kubomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro-Dar es Salaam.
Mwananchi ilizunguka maeneo mbalimbali ambayo yamekatiwa umeme na kushuhudia wananchi wakitumia mishumaa, vibatari, taa za kandiri na simu nyakati za usiku huku maeneo ya nje yakionekana kuwa na giza totoro.
Miongoni mwa kaya ambazo kwa sasa zinakaa gizani ni pamoja na ya wajane Joyce Elias (70), Zainabu Mwinyimvua (78) na jengo la biashara lenye gorofa tatu linalomilikiwa na Revy Kapinga ambaye pia ni mjane.
Mbali na nyumba za wananchi, majengo mengine yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni nyumba za ibada, vituo vya mafuta, kituo cha watoto yatima, vituo vya afya zikiwamo hospitali na zahanati pamoja na ofisi moja ya kata.
Tanesco wakata umeme chini ya ulinzi
Tanesco imeendelea kukata umeme huku mafundi wake wakifanya kazi hiyo wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ikiwa ni hatua ya awali ya wananchi hao kubomoa nyumba zao. Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao walisema wanashangaa hatua ya kukatiwa umeme wakati kesi yao bado ipo mahakamani na hivyo kulazimika kuishi gizani.
Mkazi wa eneo hilo, Rehema Kalolo alisema ni vizuri Tanesco ingesubiri uamuzi wa mwisho utakapotolewa kwa sababu mpaka sasa hawajui hatima ya nyumba zao na kwamba, anatumia kibatari kwa ajili ya mwanga wakati wa usiku baada ya nyumba yake kukatwa umeme. Alisema tangu walipokatiwa umeme hali ya uchumi imebadilika kwa sababu nje ya nyumba alikuwa akiendesha biashara zinazotegemea nishati hiyo.
Rehema alidai kuwa hawezi tena kufanya biashara hizo na kwa sasa anasubiri siku watakayobomolewa kabisa nyumba wanayoshi jambo ambalo litawaongezea umaskini.
“Tupo gizani kwa wiki sasa, Tanesco walikuja hapa wakang’oa mita zao na kuondoka. Ni giza tu eneo lote hili, tunaishi kwa hofu kubwa. Kibaya zaidi hata kazi tulizokuwa tukitegemea kuendeshea maisha hatuwezi tena kuzifanya,” alisema.
Rose Robert, mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa alisema hofu imetawala kwenye familia yao kwa sababu wanajua wakati wowote watabomolewa kwa kuwa tayari wameshakatiwa umeme. “Sina amani na sijui nitaelekea wapi kwa sababu kukatiwa umeme ni dalili kwamba wakati wowote nyumba yangu itabomolewa. Ni maumivu makali ni sawa na mtu kukuchoma mkuki kwenye kidonda.” alisisitiza.
Kiongozi wa wananchi waliowekewa X kwenye eneo la Kimara Stop Over, Ephraim Kinyafu alisema kuwapo kwa giza kwenye nyumba nyingi za wananchi waliokatiwa umeme kumesababisha kuongezeka kwa wimbi la uharifu.
Alisema kwa sasa wanashindwa hata kukutana na kuzungumzia hatima yao kwa sababu hawajui kinachoendelea zaidi ya kuwaona wafanyakazi wa Tanesco wakiendelea kukata umeme.
“Hatupingani na ujio wa maendeleo lakini walau wananchi wangekuwa wanashirikishwa, wajue ni nini kinaendelea,” alisema Kinyafu.
Alisema kuwa awali mita zilizokuwa zinapaswa kuachwa kama hifadhi ya barabara zilikuwa 60 hivyo wananchi wengi walijenga nje ya umbali huo. Hata hivyo, baadhi ya maeneo bado hayajakatiwa umeme japokuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa hofu wakisubiri hatima ya nyumba zao.
Mzee John Mlangi, mkazi wa Kimara Suka alisema tangu awekewe alama X hajui kinachoendelea japo ikitokea nyumba yake ikabomolewa atabaki hapo kwa sababu hana sehemu nyingine ya kwenda.
“Mimi sijakatiwa umeme bado, lakini huenda wakaja kukata kama walivyofanya kwa wengine, nimeshastaafu na kwa kweli sijui hatima ya maisha yangu ya uzeeni. Nilijenga nyumba hii miaka 35 imeshapita nadhani, Serikali inalo jambo la kutazama hapo,” alisema.
Kwa upande wake, Ahmad Kalolo alisema barabara hiyo ndiyo iliyovamia baadhi ya maeneo ya wananchi hasa wale waliojenga miaka mingi iliyopita wakati bado haijajengwa.
“Barabara hii imenikuta. Zamani ilipita kule upande wa pili, kwa hiyo nipo eneo sahihi ambalo sio mimi natakiwa kuvunja, Serikali inapaswa kunilipa fidia na kuvunja,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa barua ya Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, wanatarajia kufanya upanuzi wa barabara ya Morogoro umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara.
Barua hiyo ilisema kwa kuwa nyumba, ukuta, shimo la majitaka, uzio na fremu za biashara viko ndani ya hifadhi ya barabara kinyume cha sheria, wamiliki wanaagizwa kubomoa. Pia, barua hiyo iliwataka wabomoe ndani ya siku 30 kuanzia siku ya barua hiyo na wasipofanya hivyo, watalazimika kulipa gharama zote zitakazojitokeza.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamelazimika kwenda mahakamani ili kuweka zuio la ubomoaji wa nyumba hizo.
No comments:
Post a Comment