Friday, August 4

Rwanda wachagua Rais leo


Rwanda. Wananchi wa Rwanda leo Ijumaa, Agosti 4 wanapiga kura kuchagua Rais wao atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka saba ijayo.
Ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa huku mgombea wa Chama cha Rwanda Patriotic Front (RPF), Paul Kagame akitabiriwa kupata ushindi wa kishindo.
Wakati leo wananchi wakijiandaa kupiga kura tayari wananchi wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi hiyo wameshapiga kura  na taarifa za Tume ya Uchaguzi ya Rwanda zinaonyesha takribani watu 50,000 walio nje ya taifa hilo wamejiandikisha kupiga kura.
Tofauti na Tanzania, katika uchaguzi unaofanyika leo wapigakura hawatatumia mfumo wa kielekroniki bali watatumia karatasi, peni na kidole gumba.
Uchaguzi huo wa Rais ambao kampeni zake zilichukua siku 21 na kufikia tamati juzi jioni, una wagombea urais watatu ambao ni Kagame wa RPF, mgombea binafsi, Philipe Mpayimana na Dk Frank Habineza wa Chama cha Mazingira (Green Party).
Utabiri wa ushindi wa Kagame unatokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakihudhuria katika mikutano yake ya kampeni katika wilaya zote 30 za Rwanda na ukweli kwamba vyama vinane vya upinzani tayari vimetangaza kumuunga mkono.
Kagame mwenyewe ameonyesha matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo na kusema mwitikio wa Wanyarwanda unaonyesha ni jinsi gani wamejifunza kilichotokea siku zilizopita na wana haki ya kuchagua njia iliyo sahihi. 

No comments:

Post a Comment