Friday, August 4

Mbunge wa Chadema bado yuko polisi


 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amesema bado wanaendelea kumshikilia Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga na watamfikisha mahakamani baada ya kukamilisha upelelezi.
Kamanda Nyange amesema sababu za kumtia mbaroni Haonga ni kutokana na kufanya mkutano bila kibali cha polisi katika mji mdogo wa Mlowo-Mbozi na kuwahamasisha wamiliki wa malori na abiria kuandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Chiku Galawa.
Amesema Haonga alifanya mkutano huo jana Jumatano, Agosti 2 na  alihamasisha madereva wa malori, wamiliki na abiria  waende kumuona mkuu wa mkoa.
Amesema lengo la mbunge huyo kuwataka watu hao wamuone mkuu wa mkoa ni  kueleza kero yao juu ya adha ya usafiri baada polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kupiga marufuku malori kubeba abiria kutoka katikati ya mji wa Mlowo kwenda maeneo tofauti ya vijijini ambako hakuna usafiri mbadala zaidi ya malori.
“Bado hatujakamilisha upelelezi na tutakapokamilisha muda wowote tutamfikisha mahakamani na kuhusu dhamana tutafikiria kumpatia dhamana ama laa,” amesema Kamanda Nyange.
Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga amesema baada ya kupewa tarifa kwamba Mbunge wao hatafikishwa mahakamani wameanza kushughulikia suala la dhamana chini ya wakili wao Boniface Mwabukusi.
Amesema: “Tupo hapa kuandaa hati za dhamana ili aweze kutoka leo kwani wamesema hawatamfikisha mahakamani leo, hivyo wakili wetu (Boniface Mwabukusi) yupo kuandaa watu wa kumdhamini pamoja na barua ya mwenyekiti wa kitongoji na kama itashindikana kumtoa kwa dhamana leo basi tutamuomba wakili wetu twende Mahakama kuu kufungua kesi ya kudai dhamana itolewe.”

No comments:

Post a Comment