Kila Jumanne huwa nina safari ya kwenda Chang’ombe kwa ajili ya kazi fulani maalumu. Kama kawaida, Jumanne ya Agosti 15 haikuwa tofauti. Saa tatu asubuhi nikajipanga kuanza safari ya kuelekea Chang’ombe nikitokea Magomeni ninakoishi.
Safari ilikuwa nzuri hadi Ilala Boma mambo yalipobadilika. Katika hali isiyo ya kawaida magari yalisimama katika foleni kwa dakika takriban 30 kabla hazijaruhusiwa.
Baada ya kuvuka mataa ya Boma, ndipo nilielewa ni kwa nini. Ni kwamba upande wa pili wa barabara, ukivuka mataa uelekeo wa Chang’ombe, magari yalikuwa hayatembei.
Baada ya kuvuka mataa magari yalisogea mpaka usawa wa majengo ya Machinga Complex na hapo yalikwama kwa muda wa takriban saa mbili au zaidi kabla ya kuruhusiwa tena.
Haikuwa rahisi kwangu hata kidogo, ingawa nilikuwa katika gari binafsi. Nina hakika kwa wale waliokuwa katika magari ya umma – madereva na hata abiria – hali ilikuwa ngumu na walikereka zaidi.
Katika saa mbili nilizoegesha gari, nilisikiliza redio, nikibadili kila ‘station’ ninayoijua, nikachoka. Nikalaza kiti kidogo kujipumzisha, lakini miale mikali ya jua ikaniamsha. Pia nilikuwa na wasiwasi na askari kunikuta nimelala. Mwisho, nikatoka nje kupiga soga na jamaa aliyekuwa katika gari ya mbele yangu. Pia nikachoka na kuamua kurudi garini, nikisonya, na kulaani.
Wakati wote huo nilikuwa nahisi tu kuwa kuna msafara unapita, lakini wakati nikipiga soga na yule jirani yangu katika foleni ndipo aliponithibitishia kuwa kumbe mgeni wetu, Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi alikuwa anaondoka siku hiyo.
Jirani yangu aliniambia amesikia TBC matangazo ya moja kwa moja ambapo Rais John Magufuli anawaongoza Watanzania kumuaga mgeni wake ambaye pia ni mgeni wetu.
Kupata ugeni ni baraka, ndivyo tunavyoamini, lakini si jambo la busara sana kuendesha shughuli za kupokea au kumuaga mgeni katika namna ambayo shughuli za kawaida za maendeleo za watu zinalazimika kusimama.
Ninachosema ni kwamba, kungeweza kuwa na namna bora ya kupokea au kuaga ugeni bila kuwakwaza wengine.
Nasema hivi kwa nia safi na si kwa kubeza au kutotambua faida nyingi zilizopatikana kutokana na ugeni huo.
Nikipiga mahesabu ya harakaharaka ya foleni ile ya Barabara ya Kawawa (ambayo naambiwa ilifika hadi Magomeni) na katika maeneo mengine (ikiwemo Posta na Kariakoo), Barabara ya Mandela, naamini muda tuliopoteza tukiuweka katika fedha tutakuwa tumepoteza mamilioni ya fedha.
Watu wamechelewa kazini, kwenye biashara zao, kwenye mikutano na hakukuwa na matangazo ya kabla, kwamba barabara hizo zisingepitika muda huo.
Baadhi ya miadi ilibidi ivunjwe kwa sababu ya usumbufu ule. Inawezekana kulikuwa na wasafiri walioachwa na mabasi, boti au ndege. Foleni za aina ile zinaweza hata kupelekea hata vifo vya watu, kwa mfano mgonjwa, kushindwa kufikishwa hospitali mapema na kadhalika.
Waliosulubika katika foleni siyo peke yangu ninayepaza sauti. Katika mtandao mmoja wa kijamii, mtu mmoja, akiwa eneo la Uhasibu alilalamika kuwa wamezuiwa kuingia mjini. Alisema magari hayajatembea kwa saa tatu na kwamba watu wameamua kushuka kwenye mabasi na kutembea kwa mguu.
Mwingine akaandika: “Leo kwa kweli tumekomeshwa aisee. Masaa mawili na nusu gari hazitoki wala kuingia kituo cha daladala pale gerezani. Nililala, nikaamka bado hatujatoka. Unaweza ukajikuta unakosa kibarua kwa ajili ya misafara yao. Kwanza si walisema wanaenda Dodoma? Waende bwanaa,”
Mwingine akaandika: “Leo mimi ni mhanga wa tukio hili. Kwa kweli nimekasirika sana. Saa matatu katika foleni kwa ajili ya watu kutoka ikulu kwenda uwanja wa ndege tu.” Na mwingine akasema: “Yalinikuta jana wakati naenda Kariakoo. Nimekaa katika foleni masaa mawili.”
Maoni niliyoyapenda zaidi ni ya yule aliyesema: “Yaani wakati dunia ikifanya mambo mengi kuokoa muda, sisi huku tunafanya juhudi kubwa ya kupoteza muda. Fikiria vitu vingapi tumepoteza.”
Kama hali iko hivi kutokana na ziara ya rais mmoja, fikiria inakuwaje tunapokuwa na mkutano wa marais 10 wa nchi tofauti hapa Dar es Salaam na wakawa wote wanahitajika kuondoka siku moja.
Wale ambao shughuli zao zinawalazimisha kusafiri na kukatisha barabara zinazopitiwa na misafara hiyo, wanaweza kweli kwenda kuwajibika kufanya shughuli zao?
Baadhi ya watoa maoni katika mitandao waliamua kuleta siasa katika suala hili kwa kuwalaumu viongozi, jambo ambalo halina mantiki. Kinyume na lawama, viongozi wanastahili pongezi kwa juhudi za kuimarisha miundombinu ya Dar es Salaam na uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuhamishia Serikali Dodoma ifikapo 2020.
Nini cha kufanya
Hata hivyo, wakati tunasubiri ujenzi wa miundombinu hiyo umalizike – ikiwemo hizo barabara za juu (flyovers) na barabara za mwendo kasi – hatua za dharura zinahitaji kuchukuliwa kuondoa kero za foleni wakati wa misafara ya viongozi, hususan tunapotembelewa na viongozi wa nje.
Anayepaswa kuchukua hatua za dharura si Rais, bali watendaji wote wanaoratibu ratiba, protokali na usalama wa misafara hii, wakiwemo maafisa wa ikulu, vyombo vya dola na muhimu zaidi viongozi wa mkoa.
Mambo matatu yananijia haraka kichwani kuwa yangeweza kufanyika kuondoa kero ya foleni wakati wa misafara kama hii.
Kwanza, kungekuwa na utaratibu wa kusafirisha wageni hawa kwa helkopta mpaka uwanja wa ndege na kutuacha wengine tuendelee na mambo maisha yetu ya kawaida.
Nina hakika gharama za kusafirisha viogozi hawa kwa helkopta ni nyepesi sana ukilinganisha na gharama kwa uchumi wetu kutokana na watu kuchelewa kwenye shughuli zao.
Pili, kama ni lazima kutumia barabara, upo umuhimu wa kupunguza idadi ya viongozi wanaoenda kusindikiza msafara.
Yaani, kwa maana nyingine, tuachane na ule utamaduni na utaratibu wa viongozi wote wa kitaifa, mikoa, wilaya, tarafa, kata hadi mtaa kuacha shughuli zote na kwenda uwanja wa ndege kumshuhudia Rais wakati akimuaga mgeni wake au yeye mwenyewe akiondoka kuelekea safari fulani.
Kufanya hivi kutasaidia si tu kupunguza foleni ndefu za misafara, lakini pia wao wenyewe viongozi na watumishi watakuwa na muda zaidi wa kufanya kazi za wananchi, badala ya kwenda mahali ambako hawahitajiki bali kuongeza idadi.
Tatu, kama yote hayo yameshindikana, viongozi waratibu wa safari hizi watupe taarifa mapema kuwa barabara fulani zitafungwa muda kadhaa. Taarifa za aina hii zinasaidia kwa njia mbili.
Kwanza, inatusaidia kuamua kutumia barabara mbadala ambazo hazitaathirika kwa foleni kutegemeana na wapi mtu anataka kuelekea. Pili, kama hakuna njia nyingine ya kupita, walau baadhi ya watu tunaothamini muda wetu tunaweza kuamua kutotoka muda ambao tunajua barabara husika imezuiliwa.
Siku ile ya Agosti 15, ningejua hali ingekuwa vile kwamba barabara inafungwa kwasaa mbwili mpaka tatu, kwa vyovyote nisingetoka nyumbani muda ule. Ningekaa na kupunguza kazi nyingine zinazonikabili ambazo naweza kuzifanyia nyumbani.
No comments:
Post a Comment