Thursday, August 24

JPM, Mbowe wakitaniana, wafuasi watadumisha utani




Utani ni rutuba yenye kustawisha siasa bora. Mijadala ya kisiasa inapaswa kujengwa huku vicheko vikitawala. Wenye kujadiliana au kubishana wanatakiwa kuunda nyuso zao kwa tabasamu.
Lugha rahisi kueleweka na ufafanuzi wenye kuzingatia matakwa ya hoja, matamshi yenye kupingana kirafiki na kindugu badala ya ubishani wenye viashiria vya uadui, ni mbolea yenye kusimamisha nguzo za ustaarabu wa kisiasa.
Kufanikisha siasa za kistaarabu, viongozi wa juu kwenye vyama hutakiwa kuwa mfano wa kuigwa na wale wa chini yao, mwisho wafuasi huiga na kuishi ndani ya misingi ya ustaarabu wa kisiasa. Siasa zinazofanywa na wenye nyuso za furaha ni zenye kuvutia mno.
Utani, vicheko na tabasamu wakati wa mijadala, haimaanishi umakini haupo, la! Vilevile, maneno makali, mikunjo ya ndita na jazba, havibebi tafsiri ya umakini. Ukiielewa falsafa hii, utaelewa kwa nini wanasiasa wenye kufanikiwa zaidi ni wale wasioamini kwamba tofauti ya vyama ni uadui.
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini ya kidemokrasia, Nelson Mandela, alipoingia madarakani mwaka 1994, alionyesha kwa vitendo kuwa viongozi wa vyama pinzani wanaweza kuishi kwa kupingana kwa hoja lakini wakaendelea kushirikiana kujenga nchi moja.
Mandela akiongoza chama cha African National Congress (ANC), alifanya kazi na wapinzani wake, Frederik de Klerk wa National Party (NP) na Mzulu wa Inkatha Freedom Party (IFP), Mongasuthu Buthelezi.
Suala la Mandela kuwateua De Klerk na Bethelezi katika Serikali aliyoiunda, linaweza lisiwe kielelezo kikubwa kwa sababu alitii makubaliano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini jinsi ambavyo aliishi nao serikalini.
De Klerk aliteuliwa kuwa Naibu Rais kama pambo kuonesha wazungu kuwa Serikali ilikuwa ya pamoja, kwani chama chake kilipata wabunge 82 ambao ilikuwa sawa na asilimia 20. De Klerk alikubali pia kuwa naibu wa Rais Mandela kwa afya ya ujenzi wa Afrika Kusini mpya.
De Klerk alihudumia cheo hicho  pamoja na Thabo Mbeki. Mtendaji hasa alikuwa Mbeki. Mwaka 1996, De Klerk alijiuzulu na kuacha siasa kwa amani. Ushirikiano wa De Klerk na Mandela, uliziunganisha vizuri jamii za weupe na weusi.
Mandela alimteua Buthelezi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati IFP kilipata wabunge 43, sawa na asilimia 11. ANC ilishinda wabunge 252, sawa na asilimia 63, na kwa vile chama chenye wabunge wengi ndicho kinaunda Serikali, Mandela baada ya kuchaguliwa na wabunge kuwa Rais, angeweza kuvitenga vyama vingine.
Unaweza kurejea kwenye kuheshimu makubaliano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, vilevile ukweli kwamba Mandela alimhitaji De Klerk kuwaaminisha wazungu kuwa bado Afrika Kusini ni nchi yao pamoja na kuongozwa na weusi, vilevile Buthelezi alikuwa muhimu kwa ajili kuituliza jamii ya Wazulu.
Siasa za Mandela
Buthelezi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa mpinzani hasa wa Mandela. Kwanza alipinga muundo wa Serikali unaofuata mfumo wa urais (Presidential System), alitaka mfumo wa Serikali ya Kibunge (Parliamentary Democracy).
Jeuri ya Buthelezi kuwa anatoka kwenye kabila kubwa (Zulu), ilikuwa sababu ya kumpinga na kumzodoa Mandela. Kuna wakati wafuasi wa ANC na IFP walishambuliana na kuuana. Zaidi ya watu 15,000 walipoteza maisha katika mapigano ya wafuasi wa vyama.
Ni kwamba Afrika Kusini baada ya kutokomeza ubaguzi wa rangi na Mandela kuwa Rais, mpingaji mkuu wa Serikali hakuwa mzungu, isipokuwa Buthelezi. Alimzodoa Mandela kwa kushindwa kutekeleza sera za ujamaa.
Hata hivyo, Mandela alimweka karibu Buthelezi, na Februari 1997, alifanya tukio lililoshangaza wengi, alipomteua kuwa Kaimu Rais. Hata siku Mandela analihutubia Bunge na kumtangaza Buthelezi kuwa atakaimu urais, wabunge waliangua vicheko wakidhani alikuwa anamtania hasimu wake.
Wala haikuwa utani, Mandela alikuwa na safari ya Uswis katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), wakati huo pia Mbeki (Naibu Rais), alikuwa tayari Davos, Uswis kwa ajili mkutano wa WEF, hivyo Mandela alimteua Buthelezi kuwa Kaimu Rais kipindi chote akiwa nje ya nchi.
Ni rahisi kuwezekana
Kiongozi gani mwingine Afrika anaweza kumteua hasimu wake kuwa kaimu rais? Mandela aliweza kwa sababu alitambua kwamba siasa ni tamu kama ikifanywa bila presha. Alijiamini, hakuwa na wasiwasi na kiti chake.
Kumweka karibu mpinzani, kumwacha akukosoe na kumshirikisha kwenye masuala ya ujenzi wa nchi na kucheka naye, hakumfanyi awe tishio. Buthelezi na IFP yake waliporomoka umaarufu na kupoteza majimbo tisa katika uchaguzi 1999.
Bila shaka, IFP kingepata umaarufu mkubwa na kukisumbua ANC kwenye Uchaguzi Mkuu 1999 kama Buthelezi angeonekana adui na kushughulikiwa. Kitendo cha Buthelezi kushirikishwa kwenye muundo wa Serikali, vilevile Mandela kuishi naye kwa tabasamu, kilikipa hadhi kubwa ANC na kuonekana kweli ni nembo ya Taifa kwa makabila yote.
Muhimu zaidi ni kwamba jinsi Mandela alivyoishi kwa tabasamu na Buthelezi, kulijenga imani kwa jamii ya Wazulu ambao waliridhika kuwa ANC ni chama chao, hivyo IFP kupungua kuungwa kwao mkono na kabila hilo.
Vilevile tabasamu la Mandela kwa De Klerk na viongozi wengine wa NP, kuliwakaribisha wazungu na kuiona Serikali kuwa yao, hivyo kuwa watiifu kwayo. Mandela angemtenga De Klerk, wazungu wangeona wanahitaji ukombozi, hivyo wangeweza kuihujumu Serikali.
Iliwezekanaje Afrika Kusini?
Mwaka 2012, Buthelezi alitoa andiko na kuliita Mandela and I (Mandela na Mimi), kisha kuchapishwa kwenye tovuti ya Politicsweb.com, ndani yake alieleza kwa kirefu jinsi alivyofahamiana na Mandela tangu miaka ya 1950 na walivyoishi wakati wa harakati za ukombozi na baadaye kufanya kazi katika Serikali moja.
Buthelezi alisema kuwa mwaka 2002, Mandela alikiri hadharani kwamba ANC ilijaribu kukitokomeza IFP bila mafanikio, hivyo akataka chama hicho kisipuuzwe, maana kina nguvu yenye kuhitaji kuheshimiwa.
Unapata jawabu kuwa kumbe sababu ya Mandela kumheshimu Buthelezi mpaka kumteua kuwa Kaimu Rais, ni baada ya kutambua nguvu ya chama chake kisiasa, hivyo badala ya kupambana naye, akaona vema kuishi kwa tabasamu.
Utaona kuwa mwaka 2012, Buthelezi alipozungumza hayo, ilikuwa mwaka mmoja kabla ya kifo cha Mandela na alikiri kwamba kiongozi huyo alistahili heshima ya dunia kwa namna alivyoishi na wapinzani wake, akawakosoa viongozi waliofuata baada yake, Mbeki na Jacob Zuma kwamba hawakucheka naye, bali walipambana naye.
“Mfano Zuma ndiye aliyenikabili na kuniambia niachie uongozi wa IFP, ukweli Mandela alikuwa muungwana sana,” alisema Buthelezi.
Mwenyekiti wa CCM, Dk John Magufuli na wa Chadema, Freeman Mbowe wakitaniana na kuzungumza kwa lugha ya bashasha na kuelewana katika kupingana kwao, itapunguza presha kwa wafuasi wa chini na kuwafanya nao wacheke na kutaniana bila chuki.
Viongozi lazima kuonesha kwa vitendo kwamba  vyama si bora kuliko ujenzi wa nchi moja. Wathibitishe kwamba vyama ni sehemu ya utamaduni wa kidemokrasia katika kushindania uongozi wa dola lakini havibebi leseni ya kuwagawa watu.
Mwaka jana, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, walisema kuwa wao huzungumza na kupigiana simu ili kujadili mambo ya nchi na namna ya kutuliza presha za wafuasi pale joto linapopanda.
Itavutia pia kuona Rais Magufuli na Mbowe wakiwa na utaratibu wa kupigiana simu na kuzungumza kuhusu nchi itakuwa afya kwa nchi.

No comments:

Post a Comment