Wednesday, August 30

Muuguzi aua wagonjwa 90 ili awafufue


Berlin, Ujerumani. Muuguzi nchini Ujerumani anayetumikia kifungo cha maisha kwa kuwaua wagonjwa sita, imebainika aliwaua wengine 84.
Idadi ya watu aliowaua imemwingiza katika rekodi ya mwanamke aliyefanya mauaji mengi kuliko wote nchini humo.
Mwanamke huyo, Niels Hoegel (40), alifungwa mwaka 2015 baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wagonjwa sita kwa kuwachoma sindano inayosababisha moyo kusimama ghafla.
Mamlaka za nchi hiyo zimekuwa zikifanya uchunguzi wa maelfu ya vifo, ikiwamo kufukua maiti za wagonjwa waliokufa chini ya uangalizi wake katika hospitali binafsi za Delmenhorst na Oldenburg ambazo amewahi kufanya kazi.
Polisi nchini humo wameliambia Shirika la CNN kuwa, wanaamini Hoegel aliua wagonjwa 36 katika Hospitali ya Oldenburg kati ya mwaka 1999 na 2001, na wengine 48 katika Hospitali ya  Delmenhorst.
Pia, wanasema idadi ya watu aliowaua inaweza kuwa kubwa zaidi lakini ushahidi hautapatikana kwa kuwa miili mingi ilichomwa moto, hivyo si rahisi kugundua sababu ya kifo kwa kupima majivu.
Katika mwendelezo wa kesi zake, Hoegel amekiri kuwachoma sindano wagonjwa ili moyo ushindwe kufanya kazi naye ajaribu kuwafufua kwa kuuamsha.
Amesema alitamani kuona anamfufua mtu baada ya kumchoma sindano hiyo na kwamba, alifadhaika aliposhindwa kuwarudishia uhai.
Johann Kuehme, ofisa wa polisi katika Mji wa Oldenburg aliwaambia wanahabari jana Agosti 29 kuwa idadi hiyo ya vifo imewaduwaza.
"Mauaji huenda yasingekuwa makubwa kiasi hiki kama hospitali hizi zingechukua hatua kuchunguza vifo au kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu vifo hivyo ili vichunguzwe,” amesema.

No comments:

Post a Comment