Ndivyo mjane, Revy Kapinga alivyokuwa akisema huku akiangua kilio mbele ya kaburi la mumewe John Kapinga nyumbani kwake Kimara Stop Over jijini hapa baada Wakala wa Barabara (Tanroads) kuweka alama ya X kwenye jengo hilo alilokuwa akilitegemea kiuchumi.
Baada ya kilio, mama huyo aliwaomba waandishi wa habari wa Mwananchi waliokuwa naye kwenye kaburi hilo kufanya maombi huku akimuomba Rais Magufuli kumkumbuka.
Hivi karibuni, Tanroads ilisema kwamba inatarajia kubomoa nyumba zilizowekewa alama ya X katika barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvia, wakati wowote kuanzia sasa ikisema muda ambao wamiliki walipewa kufanya hivyo wenyewe umemalizika.
Huzuni na simanzi ndiyo iliyokuwa imetawala kwenye nyumba ya mjane huyo ambaye alionekana kukata tamaa huku akiwa hajui hatima ya maisha yake.
Ghorofa hilo ambalo tayari limeshakatiwa umeme na Tanesco, lina zaidi ya vyumba 50 zikiwamo fremu 30 alizokuwa amepangisha.
Revy alisema ombi lake kwa Rais Magufuli ni kumuachia jengo hilo kwa kupunguza mita zilizopimwa kutoka barabarani au kulipwa fidia ili yeye na wajane wengine waweze kuendesha maisha yao.
“Jengo hili ndilo msaada pekee wa maisha yangu na familia. Hizi ni biashara alizoniachia mume wangu, sina kingine chochote ninachokitegemea na kilio changu naomba kimfikie Rais wangu, atuhurumie,” alisema.
Hali halisi nyumbani
Saa sita mchana, waandishi wa Mwananchi walifika nyumbani kwa mjane huyo ili azungumzie hatima yake baada ya ghorofa hilo kuwekewa alama hiyo ya X.
Haikuwa kazi rahisi. Mama huyo alikuwa akilia kwa uchungu jambo lililomfanya mtoto wake kuwazuia waandishi kuzungumza naye.
Hata hivyo, baada ya dakika 10, mtoto huyo alituruhusu tuingie kwenye eneo la mapumziko ili kumsubiri mzazi wake. Haikuchukua muda mrefu kwa mama huyo kufika.
“Karibuni sana wanangu,” alitukaribisha kwa sauti ya unyonge uliotokana na kilio alichokuwa nacho.
Baada ya makaribisho tulimuuliza kuhusu kilio hicho ilhali tangazo la kubomolewa kwa nyumba hizo limetolewa siku nyingi naye akasema awali, Tanroads walimuwekea X kwenye nusu ya majengo yake.
“Walipokuja mara ya kwanza waliweka kwenye majengo mengine wakaliacha hili ghorofa, nashangaa jana jioni wameliweka hili pia kwa kweli naumia,” alisema.
Alisema kwa kuwa hakutaka kushindana na Serikali, alitii na kuvunja majengo ya awali yaliyokuwa yamewekwa X hiyo mara ya kwanza na kuhamishia biashara zake kwenye ghorofa hilo na kwamba, bomoabomoa hiyo ya awali, ilimgharimu zaidi ya Sh20 milioni.
“Nilibomoa kwa sababu naamini Rais wangu anataka kutuletea maendeleo na moyoni mwangu nilishukuru Mungu kwa sababu ghorofa hili lilikuwa limesalimika, sijui hata nisemeje mwenzenu,” alizungumza huku akifuta machozi.
Haikuwa kazi rahisi kumsikiliza mama huyo ambaye alisema anatamani mumewe, angekuwa hai wakati huu ili walau amsaidie akisema tangu jana alipopata taarifa za kubomolewa kwa jengo hilo alilotarajia kwamba lingesalimika, hali yake ya afya si nzuri kutokana na presha iliyomkumba, “Wanangu naumwa, presha yangu haipo sawa niombeeni,” alisema.
Alisema wamekuwa katika eneo hilo ambalo alisema lilipatikana kisheria tangu mwaka 1990.
Alisema kuwa majengo hayo yalijengwa baada ya mumewe Kapinga kustaafu na kulipwa fedha za mafao yake.
“Fedha yote ya mafao ya mume wangu ilimwagwa pale, alifanya hivyo kwa sababu alijua anaandaa maisha yangu na wanangu,” alisema.
Alisema mume wake huyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uchumi na Kilimo la CCM (Sukita).
Baada ya mazungumzo hayo, aliomba waandishi waelekee kwenye kaburi la mumewe kwa ajili ya maombi.
“Tulisogea taratibu na tulipofika, mama huyo alituonyesha eneo ambalo yeye mwenyewe atazikwa siku yake ikifika,” anasema mwandishi wa gazeti hili.
“Hili ndilo kaburi la mume wangu, mie pia nitalala hapa pembeni yake. Wanangu naomba muongoze maombi,” alisema mama huyo.
Waandishi na mama huyo walifanya maombi mbele ya kaburi la mumewe kwa dakika 15 huku mwongoza maombi akikemea pepo la kubomolewa kwa jengo hilo lishindwe.
Baada ya maombi, mama huyo alionekana kufarijika na akamkumbatia muongoza maombi na kufuta machozi yaliyokuwa yakimtoka wakati wote ibada hiyo ilipokuwa ikiendelea.
Revy alisema anaamini kabisa kwamba Mungu atamsaidia kwenye suala hilo na kwamba kuna siku litakwisha.
Umeme wakatwa
Wakati tukiwa bado nyumbani kwake, wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), walifika katika jengo hilo na kukata umeme hali iliyowalazimu baadhi ya wafanyabishara hasa zinazotegemea nishati hiyo, kufunga biashara zao na kuondoka.
Wakizungumza na waandishi wetu, baadhi ya wafanyabishara hao walisema hali ya uchumi itayumba kwa sababu walikuwa wakilitegemea zaidi jengo hilo kwenye biashara zao.
“Binafsi sitaendelea kufanya biashara kwa sababu nategemea umeme japo wenzangu wanaweza kuendelea na jioni wakatumia taa,” alisema Neema Adolf mfanyabishara wa vifaa vya ofisini.
Aliiomba Serikali kupunguza mita kutoka barabarani hadi kwenye majengo kwa sababu awali ilikuwa ni mita 60 tofauti na mita 121.5 za sasa.
Ghorofa jingine lawekwa X
Wakati mjane huyo akilia, Tanroads waliweka alama ya X kwenye jengo jingine la ghorofa nane linalomilikuwa na Isack Kalato, makazi wa Kimara Stop Over.
Kalato alisema alitumia miaka 10 kujenga jumba hilo na kwamba ndilo alilokuwa akilitegemea kiuchumi. “Nilianza kujenga ghorofa nane na sasa nilikuwa naongeza nyingine tatu. Nasikitika Serikali inataka kubomoa wakati nilifuata sheria na taratibu zote zilizowekwa,” alisema.
Alisema angependa kujua namna mita hizo zinavyopimwa kutoka barabarani kabla ya hatua ya kulibomoa kuanza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stop Over, Magreth Mugyabuso alisema wanatarajia kufanya kikao cha kutathmini hali halisi tangu X zilivyowekwa hadi sasa ili kuona ni kwa kiasi gani wananchi wameathirika.
“Tunataka kuona namna tunavyoweza kusaidia hasa kaya zilizoathirika zaidi. Kuna wajane na wazee wasiojiweza kwa hiyo tutakutana na wananchi,” alisema.
No comments:
Post a Comment