Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya elimu ya rushwa kwenye Mabasi ya Mwendo Kasi (Udart), Mbungo amesema viongozi wa aina hiyo nao ni wala rushwa.
“Viongozi wengine ni tatizo kwa sababu kama hawawezi kukemea rushwa na kuipiga vita ni wala rushwa tu hivyo lazima wafichuliwe na hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa,”amesema.
Mbungo ambaye ameapishwa leo na Rais John Magufuli amesema madhara ya rushwa ni makubwa na kwamba, yanachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo.
“Sisi Takukuru ni vikundi vya askari washambuliaji mbele kabisa, ninyi raia na idara nyingine za Serikali ni vikundi vya msaada ambao lazima mtoe ushirikiano kuhusu masuala ya rushwa,”anasema.
Amesema kuwa taasisi hiyo itaendalea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa na kwamba, kampeni ya elimu kwenye mabasi hayo itaweza kuwafikia zaidi ya watu milioni sita kwa mwezi, kutokana na ukweli kwamba mabasi hayo husafirisha watu 200,000 kwa mwezi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Angela Kairuki amesema kila mmoja anawajibu wa kushiriki kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kwamba, ni jukumu la Takukuru kuhakikisha kuwa elimu inawafikia wananchi wote.
Amesema mbali na elimu kutolewa kwenye mabasi hayo, ipo haja kwa viongozi hao kuona namna ya kuisambaza kwenye vyombo vingine vya usafiri ikiwamo pikipiki na ndege.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando amesema wanaendelea kupambana na rushwa kwenye mkoa huo na kwamba, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wamefanikiwa kuokoa Sh 7941.4 zilizokuwa zikipotea kwa sababu ya rushwa.
No comments:
Post a Comment