Saturday, August 5

Mbunge wa Tarime akamatwa, aachiwa


Kamatakamata ya wabunge wa upinzani imeendelea na jana ilimkumba John Heche wa Tarime Vijijini (Chadema), ambaye alishikiliwa na polisi kwa saa sita na kuachiwa akidaiwa kutoa kauli za uchochezi bungeni na kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Sirari wilayani Tarime.
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema jana kuwa licha ya kumwachia, kesho (Jumapili) atatakiwa kuripoti tena polisi.
Kukamatwa kwa Heche, kunafanya wabunge wa Chadema waliokamatwa na polisi katika kipindi cha siku 30 zilizopita kwa makosa mbalimbali ikiwamo uchochezi na kufanya mikutano bila kibali, kufikia sita.
Wengine waliokamatwa ni, Halima Mdee Julai 4 kwa madai ya kumkashifu Rais John Magufuli katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Mdee alifuatiwa na Zubeda Sakuru (Viti Maalumu) na Cecil Mwambe wa Ndanda waliokamatwa Nyasa mkoani Ruvuma Julai 15 wakiwa na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji pamoja na viongozi wengine watano kwa tuhumu za kufanya mkusanyiko usio halali.
Mbali na hao, pia yumo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyefuatia kukamatwa Julai 20 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa tuhuma za uchochezi katika mkutano wake na wanahabari
Baada ya Lissu alifuata Pascal Haonga (Mbozi) aliyekamatwa Agosti 2, akidaiwa kufanya mkutano bila kibali katika eneo la Vwawa Mjini.
Akizungumza na mwandishi wetu muda mfupi baada ya kuachiwa na polisi, Heche alisema alishikiliwa kwa makosa mawili; kutoa kauli ya kuhamasisha zao la bangi liwe la biashara kama ilivyo mirungi nchini Kenya na kuhamasisha wananchi wakavamie mgodi, kauli aliyoitoa akiwa bungeni.
“Nilikwenda polisi mwenyewe saa nne asubuhi (jana) baada ya kusikia katibu wangu ameitwa, nilipofika nilisalimia vizuri na askari na wakanieleza kwamba afadhali nimefika, lakini wakati hayo yakiendelea ghafla niliona idadi ya polisi ikiongezeka na nikaambiwa nipo chini ya ulinzi,” alisema Heche.
Alisema baada ya hatua hiyo watu wake wa karibu walianza kufanya utaratibu wa dhamana na kufanikiwa kupata na polisi walimweza kwamba anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo kesho saa nne asubuhi kwa ajili kuandika maelezo.
Hata hivyo, Heche alisema nyuma ya pazia ya kukamatwa kwake ni shinikizo la kisiasa linalofanywa na watu fulani wa Tarime kwa lengo la kumkomoa ili asitekeleze vyema majukumu yake.
“We mambo yametokea Machi na ishu nyingine nimezingumza bungeni eti leo wanakuja kunikamata. Nawaambia siwezi kunyamazishwa katika kutetea masilahi ya wananchi wangu. Nitahakikisha nitaendelea kuwapigania hadi wanufaike na rasilimali zao,” alisema.
Alisema polisi bado wanaishikilia simu yake moja ya mkononi kwa lengo la kuichunguza.
Awali, Mlimi Zablon ambaye ni katibu wa Heche alisema licha ya kumshikilia mbunge huyo pia walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi uliochukua takribani saa moja.
Katibu wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alilaani hatua hiyo akidai jeshi la polisi limekiuka Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge pamoja na Ibara ya 100, juu ya kinga aliyonayo mbunge.
“Inawezekanaje mbunge akamatwe kwa kauli aliyotoa ndani ya Bunge? Kwa hivyo tunalaani na tunamtaka Spika wa Bunge atoe tamko la kukamatwa kwake dhidi ya kauli aliyoitoa akiwa bungeni,” alisema Mrema.
“Kauli alitoa Februari iweje leo ndiyo wamkamate? Hali hii hatuwezi kukubaliana nayo, kwa sasa wanamshikilia Heche lakini wanasema wanamtafuta na Ester Matiko waliyekuwa naye katika mkutano huo,” alidai. Hata hivyo, polisi haijatangaza kumtafuta mbunge huyo wa Tarime Mjini.

No comments:

Post a Comment