Mashambulio mawili ya kigaidi yaliyohusisha washambuliaji kuvurumisha magari kwenye umati wa watu yalitokea katika eneo la Catalonia, nchini Uhispania.
Hapa chini ni mambo tunayoyafahamu kufikia sasa.
Nini kilitokea?
Alhamisi alasiri, mwendo wa saa 16:50 saa za Uhispania (saa kumi na moja kasoro dakika kumi Afrika Mashariki) gari jeupe lilivurumishwa kwenye umati wa watu katika eneo la kitalii la Las Ramblas, eneo maarufu la kitalii katikati mwa Barcelona lenye kinjia cha umbali wa kilomita 1.2. Eneo hilo lilikuwa limejaa watalii.
Dereva wa gari hilo anadaiwa kuliendesha kwa kupindapinda na kujaribu kuwagonga watu wengi zaidi katika eneo la wapita njia. Wengi walianguka na wengine wakakimbilia usalama madukani na kwenye migahawa.
Watu 13 walifariki na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Mshambuliaji alitoroka kwa miguu.
Polisi wa Uhispania wameeleza shambulio hilo kuwa la kigaidi.
Shambulio la pili lilitokea vipi?
Saa nane baadaye, gari aina ya Audi A3 lilivurumishwa hadi kwenye wapita njia katika mji wa Cambrils, 110km (maili 68) kusini magharibi mwa Uhispania.
Mwanamke mmoja alijeruhiwa vibaya na baadaye akafariki akipokea matibabu hospitalini.
Afisa wa polisi pia alijeruhiwa.
Gari la washambuliaji hao lilipinduka na watu watano wakatoka nje, baadhi wakiwa wamevalia mikanda bandia ya kujilipua.
Wote walipigwa risasi na kuuawa na maafisa wa polisi. Wanne walifariki papo hapo na wa tano akafariki baadaye.
Maafisa wanaamini kuna uhusiano kati ya mashambulio hayo ya Las Ramblas na Cambrils.
Kuna mshukiwa amekamatwa?
Alhamisi, mtu mmoja kutoka eneo la Melilla linalomilikiwa na Uhispania lakini linapatikana Afrika alikamatwa aktika eneo la Alcanar. Raia wa Morocco pia alikamatwa Ripoll. Miji yote miwili inapatikana jimbo la Catalonia, ambapo unapatikana mji wa Barcelona.
Stakabadhi za raia wa Morocco Driss Oubakir, 28, inadaiwa zilitumiwa kukodisha gari lililotumiwa kushambulia Las Ramblas lakini taarifa katika vyombo vya habari zinasema kuna uwezekano stakabadhi zake ziliibiwa na kutumiwa bila yeye kufahamu.
Polisi pia wanamtafuta kaka mdogo wa Driss Oubakir, Moussa Oubakir, 18, anayetuhumiwa kuwa mshambuliaji aliyehusika shambulio la Las Ramblas, vyombo vya habari Uhispania vinasema.
Ijumaa, polisi walitangaza kwamba wamemkamata mtu mwingine eneo la Ripoll. Haijabainika iwapo alihusika katika mashambulio hayo.
Kumetokea visa vingine?
Alhamisi jioni, saa 19:30 hivi, gari liliendeshwa na kuwagonga maafisa wa usalama waliokuwa kwenye kizuizi viungani mwa mji wa Barcelona.
Gari hilo baadaye lilipatikana likiwa na mwanamume aliyekuwa amefariki humo ndani.
Wizara ya mambo ya ndani ilikanusha taarifa za awali kwamba aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Maafisa hawajafutilia mbali uwezekano kwamba kisa hicho kilihusiana na shambulio la Las ramblas, lakini uchunguzi bado unaendelea.
Jumatano usiku, mlipuko uliharibu kabisa nyumba moja lAlcanar, 200km kusini mwa Barcelona, na kuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine saba.
Waathiriwa walitoka wapi?
Wanatoka mataifa mengi duniani, na kufikia sasa watu kutoka mataifa 34 wametambuliwa.
Majeruhi wanatoka Ireland, England, Ufaransa, Australia, China, Pakistan, Venezuela, Algeria, Peru, Ujerumani, Uholanzi, Ugiriki, Hong Kong, Taiwan, Ecuador, Marekani, Argentina, Romania, Cuba, Austria na Ufilipino.
No comments:
Post a Comment