Wednesday, August 9

Magufuli awafitini wabunge wa upinzani


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaweka katika mtego wabunge watano wa vyama vya upinzani katika majimbo yao kutokana na kauli za mafumbo alizotumia katika ziara mbalimbali ambazo amekuwa akizifanya.
Mtego unaowakabili ni ama wachague kuhamia CCM au wabakie upinzani lakini wananchi wasiwakubali tena katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.
Rais Magufuli ambaye alifanya kazi hiyo ya kichama kupitia ziara za uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kiserikali mikoani, alitumia kauli kama “Huyu ingawa ni upinzani lakini damu yake ni CCM.”
Mbali ya kauli hiyo ambayo imewafanya baadhi yao kuonekana kama ni ‘CCM B’, akiwa katika majimbo yanayoshikiliwa na upinzani, kila alipopokea kero kutoka kwa wananchi, Rais Magufuli alichomekea kauli za kuwabeza au kuwataka wananchi wasifanye tena makosa.
Lakini pamoja na kuchomekea maneno hayo, katika ziara zake Rais Magufuli amekuwa akisisitiza  kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote bila kubagua vyama, dini au makabila yao, akisema maendeleo hayana vyama.
Wabunge walioingizwa mtegoni katika majimbo yao ni; Magdalena Sakaya (Kaliua - CUF), Kasuku Bilago (Buyungu - Chadema), Mussa Mbarouk (Tanga Mjini - CUF) Vedasto Ngombale (Kilwa Kaskazini - CUF) na Saed Kubenea Ubungo - Chadema).
Alivyowatega
Julai 23, Rais Magufuli alimpongeza Sakaya kwa ushirikiano wake katika shughuli za maendeleo huku akisema ingawa kimwili mbunge huyo ni CUF, lakini damu yake na roho yake ni vya CCM.
Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kaliua, Tabora wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Kaliua – Kazilambwa, kwenye Uwanja wa Kasungu.
Dk Magufuli alisema Sakaya amekuwa akifanya kazi nzuri za maendeleo katika kutekeleza ilani ya CCM, bila kuwabagua kwa itikadi ya vyama vyao na akawataka wanaCCM kushirikiana naye.
“Mheshimiwa Sakaya ukimwangalia mwili wake ni mwana-CUF, lakini damu yake na roho yake ni mwana CCM. Inawezekana siku moja akahamia CCM. Ni bora kuwa na mwanaCUF, au mwana Chadema, au mwana-ACT anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana CCM anayefanya kazi za chama kingine. Si mmenielewa? Mimi najua maana hata wakati wa kampeni niliyaona.”
Mbali na Sakaya ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa CUF upande wa mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, Rais Magufuli, Julai 22, mwaka huu alimshtaki Bilago kwa wapigakura wake kwamba, wananchi wa eneo hilo wanateseka kutokana na makosa ambayo waliyafanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akiwa katika Jimbo la Buyungu, Rais Magufuli aliwapiga vijembe wapigakura akisema  mbunge wa hapo (Bilago), aliwaahidi wananchi kwamba angemaliza suala la maji na kuwahoji, “Leo amelimaliza?” akajibiwa badooo... kisha akasema ndiyo mjifunze sasa.
Kutoka na kauli hiyo ya Rais, Bilago aliliambia gazeti hili jana kwamba ilimlazimu kufanya ziara katika kata zote 13 za jimbo lake ili kujitetea mbele ya wapigakura wake. Alisema Rais Magufuli alikosea kuwaambia wananchi wasimchague tena katika uchaguzi ujao kwa kigezo cha kero ya maji kwani kazi ya mbunge siyo kupeleka maji, umeme wala kujenga barabara.
“Wapo walionipigia simu wakihoji juu ya kauli hiyo ya Rais, nikawaelewesha, wengine walielewa palepale na wengine ilibidi niwazungukie kwenye kata zangu kuwaelewesha, wananchi wanatakiwa kujua mbunge hawezi kuleta maji, mbona mbunge wa CCM hakuwaletea maji? Hili ni tatizo la utawala uliopo,” alisema.
Mbali na Bilago, siku tatu zilizopita akiwa Tanga mjini, Rais Magufuli alimpongeza Mbarouk kwa kutumia udhaifu wa CCM kushinda ‘ili baadaye aweze kuhamia CCM.’
Kabla ya kauli hiyo, Mbarouk alimwambia Rais kuwa milango ya kuingilia kwenye nyumba ya kuwatumikia wananchi iko mingi kwa hiyo maendeleo ya wananchi yasihusishwe na tofauti za vyama vyao kwa sasa.
Hata hivyo, Rais Magufuli alifafanua kauli hiyo kwa kumkaribisha ndani ya CCM kupitia mlango wake mkubwa.
“Mimi nakubaliana na mbunge wenu, kwamba milango ya kuingia kwenye nyumba iko mingi, nikajua linyumba ni li-CCM kwa hiyo anatafuta (Mbarouk) njia ya kuingia kwenye linyumba la CCM ambalo ni likubwa, nyumba ya wengi,” alisema.
“Kwa hiyo nyumba ipo na unakaribishwa kuingia kwenye nyumba hii ya CCM,” Rais Magufuli alimkaribisha huku mbunge huyo akisimama alipokaa na kutoa heshima kwa Rais.
Lakini jana, Mbarouk alisema yeye bado ni CUF na hafikirii kuingia nyumba ya CCM kutokana na imani iliyojengwa na wananchi wa jimbo lake kupitia tiketi ya CUF.
“Najua Rais ananihitaji sana CCM na baada ya kauli yake yaliibuka makundi mawili; kundi lililoamini ni utani na lingine ndani ya chama wakihofia usaliti. Maneno ya kunituhumu kwa wapinzani ndani ya chama yalianza kutolewa lakini nikawatoa hofu kwamba kimwili na kimoyo ni CUF,” alisema Mbarouk.
Machi 3, mwaka huu, Rais Magufuli alimuweka katika wakati mgumu Ngombale wa Kilwa Kaskazini mbele ya wapigakura wake baada ya kumtaka achangie angalau Sh15 milioni kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, lakini mbunge huyo akasema hawezi kutoa ahadi ambayo hataitekeleza.
Tukio hilo lilitokea eneo la Somanga Wilaya ya Kilwa wakati Rais aliposimama kuwasalimia wananchi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Kusini.
Katika tukio hilo, Rais Magufuli alikuwa akimuuliza maswali ya mtego mbele ya wapigakura, huku akisisitiza umuhimu wake kama mbunge kuchangia ujenzi huo. Rais aliahidi kuchangia Sh20milioni.
“Jamani si mnataka na mimi nichangie? Sasa na mbunge achangie. Aseme anazipeleka wapi hizo (fedha za mfuko wa jimbo)? Sasa wewe umetoka Dar es Salaam unapitia hapa Somanga, unaenda unazitoa tu huko na hapa wana shida ya hospitali. Huoni kama unawaonea? Sasa mimi ngoja nijitolee mwenyewe, ila wananchi wanajua,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa.
Jana, mbunge huyo alisema kauli hiyo ya Rais ilimlazimu kufanya mikutano katika kata za Kinjumbi na Namayuni kuwaweka sawa wapigakura wake.
“Wapo wananchi ambao hawakuelewa pale na ndiyo maana niliamua kufanya mikutano, maana ilionekana Rais ndiye mwenye msaada na mimi sina umuhimu, niliwaeleza kuwa fedha za mfuko siyo za mbunge na zina utaratibu wa kutolewa, nina kata 13, vijiji 54, haikuwezekana kutoa Sh15milioni kati ya Sh36 milioni zilizokuwa zimebakia,” alisema.
Ngombale alisema Rais aliamua kutumia mbinu hiyo kuzunguka katika majimbo mbalimbali ya wabunge wa upinzani ili kuwadhoofisha kwa wapigakura wao, jambo ambalo halitafanikiwa.
Pia, katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Aprili 15, Rais Magufuli alitumia staili nyingine ya kumshtaki kwa wananchi Kubenea wa Ubungo.
Kwa kuwa chuo hicho kipo katika jimbo hilo linaloongozwa na mbunge huyo wa Chadema alitarajiwa kwamba angehudhuria sherehe hizo za ufunguzi, lakini Rais Magufuli alipomuulizia ili azungumze chochote kwa niaba ya wananchi wake, hakuwapo.

No comments:

Post a Comment