Friday, August 18

JAFO AAGIZA MKANDARASI WA MRADI WA MAJI ITISO ASAKWE


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe. Selemani Jafo amemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Chamwino Athumani Masasi kumtafuta mkandarasi wa mradi wa maji Itiso ili akamilishe mradi huo haraka kabla ya kuchukuliwa hatua.

Akizungumza leo katika ziara yake ya kukagua mradi huo, Jafo amesema mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Audancia anatakiwa kurudi eneo la mradi haraka kukamilisha kama mkataba wake unavyoelekeza.

“Mmtake arudi haraka hapa kwenye eneo la mradi au kama ikishindikana achukuliwe hatua za kisheria kwa kukamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani kutokana na kushindwa kutekeleza mkataba,”amesema Jafo. 

Amesema Mkandarasi huyo ametoweka eneo la mradi huku akiwa amefunga mabomba yenye ubora wa chini kwenye njia kuu (Main line) kinyume cha mkataba.Ameeleza kuwa mkandarasi huyo amelaza mabomba ya Class B(PN 6) badala ya bomba za Class C(PN10) jambo ambalo 

limesababisha mradi huo kushindwa kufanyakazi kwa kuwa mabomba yaliyofungwa yameshindwa kuhimili msukumo wa maji.Kadhalika, Jafo pia ameagiza mkandarasi mshauri wa mradi huo O&A Company LTD kutafutwa kwani ameshindwa kusimamia mradi huo ipasavyo na kuruhusu kazi hiyo ifanyike kinyume cha mkataba na kuruhusu mkandarasi atoke eneo la mradi wakati vituo vinne havitoi maji kati ya vituo kumi vya mradi. 

Hata hivyo Jafo ametoa onyo kwa wakandarasi washauri na wakandarasi wa ujenzi wa maji ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao kwamba hivi sasa kazi zilizo chini ya Ofisi ya Tamisemi watazisikia kwenye bomba.

“Tutakuwa tumebaini makampuni yote yanayofanya kazi kwa ubabaishaji na kutoyapatia kazi tena za usimamizi na ujenzi katika halmashauri zote,”amesema Naibu Waziri Jafo.

Jafo ameagiza kasoro zote za mradi huo zirekebishwe na ifikapo Septemba 15, mwaka huu mradi huo uwe umekamilika.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Seleman Jafo akizungumza na wananchi nakutoa maelekezo watendaji wa Halmashauri ya Chamwino katika mmoja ya kituo cha kuchotea maji kwenye mradi wa maji Itiso. 
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Seleman Jafo akizungumza na wananchi nakutoa maelekezo watendaji wa Halmashauri ya Chamwino katika mmoja ya kituo cha kuchotea maji kwenye mradi wa maji Itiso. 
Mbunge wa Chilonwa Joel Mwaka akimkaribisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo kuzungumza na wananchi katika mradi wa maji Itiso.

No comments:

Post a Comment