Akizungumza na waandishi wa habari leo(Jumatano), Makamu Mwenyekiti wa IEBC, Consolata Maina amesema kuweka hadharani matokeo ya kura za urais ni sehemu ya kazi yao.
Maina ametoa kauli hiyo kufuatia hoja ya Nasa iliyoitaka IEBC isimamishe kuweka hadharani matokeo, wakati mgombea wa Jubilee Uhuru Kenyatta akiwa tayari anaongoza kwa kura milioni 1.2.
Maina amewaambia waandishi kwamba wao wana wajibu kwa wananchi wa Kenya na kufanya kazi kwa uwazi. Pia, amesema kwa uwazi huo unaviwezesha hata vyombo vya habari kupata taarifa za uhakika na kuwaeleza wananchi wanaosubiri matokeo hayo.
Amesema kuonyesha matokeo hayo pia kunakwenda sambamba na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba kura zilizotamgazwa kwenye vituo vya kupigia kura zitakuwa ndio uamuzi wa mwisho.
Kabla ya tamko hilo, mgombea wa Nasa Raila Odinga amewaambia waandishi wa habari kwamba matokeo ya kura za urais yanayotangazwa na IEBC ni 'kazi iliyofanywa' na kompyuta.
Odinga amesema matokeo yanayoendelea kutangazwa na IEBC, hayaonyeshi matakwa ya wapiga kura ,akitaka tume hiyo ionyeshe fomu namba 34A na 34B ili kuthibitisha matokeo yanayotangazwa.
Madai hayo ya Odinga anayatoa ikiwa ni saa chache zimepita baada ya wakala wake mkuu Musalia Mudavadi na mwanasheria wa Nasa, James Orengo kutoa madai kama hayo walipozungumza na wanahabari eneo la Bomas.
No comments:
Post a Comment