India inaonekana kukabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe baada ya watu 1,094 kuthibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa huo katika kipindi cha miezi minane iliyopita, taarifa rasmi ya serikali imesema.
Katika wiki tatu zilizopita, idadi ya vifo imekuwa juu sana, ambapo watu 342 wamefariki.
Jumla ya visa 22,186 vya maambukizi ya ugonjwa huo vimeripotiwa nchini humo.
Idadi ya watu waliofariki mwaka huu ni mara nne zaidi ya idadi iliyoripotiwa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2016 ambapo visa vya ugonjwa huo vilikuwa vimeshuka sana.
Jimbo la Maharashtra magharibi mwa nchi hiyo ndilo lililoathirika zaidi ambapo waliofarikini ni 437 kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya.
Jimbo hilo linafuatwa na jimbo jirani la Gujarat lililoshuhudia vifo 297.
India ilikabiliwa na mlipuko mbaya wa homa hiyo miaka miwili iliyopita ambapo zaidi ya watu 1,900 walifariki.
Lakini visa vilishuka mwaka 2016 ambapo ni watu 265 waliofariki, lakini mwaka huu visa vimeongezeka tena.
Mlipuko mbaya zaidi wa homa hiyo nchini humo ulitokea 2009-2010, ambapo watu 50,000 waliambukizwa na wengine 2,700 kufariki kote nchini humo.
Dkt Sanjay Gururaj, mkurugenzi wa kimatibabu katika hospitali ya Shanthi, ambayo ni hospitali ya kibinafsi, amesema si lazima kwa hospitali za kibinafsi kupiga ripoti kuhusu visa vya maambukizi ya homa hiyo kwa serikali.
"Takwimu za serikali kwa hivyo zinaweza kuwa ni kionjo tu," amesema.
Homa ya nguruwe ni nini?
- Ni ugonjwa wa kupumua unaosababishwa na virusi ya influenza aina A, vinavyofahamika kama H1N1
- Chanzo chake ni kwenye nguruwe, lakini sasa huambukiza binadamu na huenezwa kwa kupiga chafya au kukohoa.
- Dalili za ugonjwa huo zinakaribiana na za homa ya msimu - homa kali, kukohoa, maumivu kooni, maumivu mwilini na mzizimo.
- Wanaoathirika zaidi huwa wajawazito, watoto wa chini ya miaka mitano, wazee wa zaidi ya miaka 65 na wale wenye matatizo mengine ya kiafya.
- Virusi hiyo vilitambuliwa mara ya kwanza nchini mexico mwaka 2009 na vikaenea upesi maeneo mengine duniani.
No comments:
Post a Comment