WATU 469 wamefungwa vifungo vya muda mrefu kutokana na kujihusisha na vitendo vya ujangili kwenye mapori tengefu, mbuga na hifadhi za wanyama nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alitoa takwimu hizo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika wizara hiyo katika kipindi cha mwaka moja kuanzia Julai 2016 hadi Juni mwaka huu.
Profesa Maghembe alisema wizara hiyo, imepata mafanikio makubwa kutokana na kufanya doria zaidi ya 350,000 kuzunguka kwenye mapori ya akiba, tengefu, hifadhi na mbuga za wanyama.
Alisema doria hizo zimesaidia kuwakamata watuhumiwa wa ujangili 7,085 na kuwafungulia kesi zaidi ya 2,097, ambapo kesi 276 zenye watahumiwa 469 zimekamilika na waliobainika wakatozwa faini Sh milioni 452. Aliongeza kuwa katika kesi nyingine 262 zenye watuhumiwa 472, zilikamilika na wahalifu walihukumiwa kwenda jela kifungu cha muda mrefu cha kuanzia miaka 20, 25 hadi 30.
“Pia wakati wakifanya doria walikamata zaidi ya silaha za aina mbalimbali 395 zikiwamo SMG 25, G3 1, rifle 27, SG 38, bastola 2 na magobore 262,” alisema. Aliongeza: “Pia askari walikamata jumla ya risasi 1,478 na magazini mbili za SMG zenye rasasi 11, mikuki 11, magunia ya mkaa 635, magogo 5,500 na magari 26, pikipiki 68, baiskeli 228, mitungi 265 na ng’ombe 88,435 kwa kuchungwa ndani ya hifadhi,” Kuhusu kupungua mauaji ya tembo, Waziri Maghembe alisema katika Mpango wa Ufuatiliaji wa Vifo vya Tembo umebaini kwamba mauaji ya tembo yamepungua Selous, Mikumi, Ruaha, Katavi na Tarangire na vifo 84 vimepungua, ambavyo vimesababishwa na mambo mbalimbali. Kupungua huko ni sawa ni asilimia 45, ukilinganisha na mwaka 2016/15 ambapo vilikuwa vingi zaidi.
No comments:
Post a Comment