Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea harakati za ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Hbari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Omar Hassan Omar akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hayupo pichani ramani ya Uwanja wa Mao Tse Tung utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake.
Balozi Seif katika picha ya pamoja na Uongozi wa ngzi ya juu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na wahandisi wa nujenzi wa uwanja wa michezo wa Mao Tse Tung.
Balozi Seif akiagana na Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuala ya Utamaduni Chimbeni Kheir baada ya kuangalia harakati za ujenzi wa uwanja wa michezo wa Mao hapo Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Harakati za ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Mao Tse Tung uliopo Mpirani Kikwajuni Mjini Zanzibar zinaendelea karibu Miezi Miwili sasa chini ya Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya Zhengtai Group ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Ujenzi huo unafuatia msada mkubwa ulioidhinishwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa Serikali ya Zanzibar katika azma ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa pande hizo mbili ukizingatia heshima uliopewa Uwanja huo wa kuitwa jina la Muasisiwa Taifa la China Hayati Mao Tse Tung.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kutembelea Uwanja huo kujionea harakati za ujenzi huo kazi ambayo inaonyesha mafanikio mazuri.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Omar Hassan Omar alisema eneo hilo litakuwa na Viwanja Viwili Vikubwa vya chezo wa Soka, viwanja vyengine vidogo vya Michezo ya ndani pamoja na eneo maalum la Mazoezi.
Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba Moja ya Viwanja hivyo utajumuisha Majukwaa Mawili ya watazamaji ambapo mipango ya baadae Wizara inayosimamia Michezo itafikiria kuweka Vibaraza ili kuwapa fursa nzuri watu kutazama michezo kwa utulivu zaidi.
Alieleza kwamba Uwanja huo utakaokuwa wa Kijamii zaidi tofauti na viwanja vyengine vinavyotoza viingilio vikubwa unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani Milino Tano sawa na Shilingi Bilioni 12 za Kitanzania.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma alisema Serikali imezingatia mambo muhimu yaliyohitajika kufanywa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo ili kuwaondoshea usumbufu wajenzi wa Mradi huo.
Waziri Rashid alisema mahitaji hayo muhimu ilikuwa ni pamoja na huduma za maji, huduma za umema pamoja na ulinzi wa vifaa na mali za Kampuni inayojenga Uwanja huo ya Zhengtai Group.
Naye kwa upande wake Mkuu wa Wahandisi wa ujenzi wa Uwanja wa MaoTse Tung kutoka Kampuni ya Zhengtai Group ya Nchini Bwana Ligen Zhang alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kazi hiyo itaendelea kutekelezwa ili imalizike kwa wakati ulipangwa.
Hata hivyo Bwana Ligen alisema licha ya changamoto chache zilizojichomoza ikiwemo rasilmali ya mchanga lakini juhudi zitachukuliwa katika kuona mradi huo unakwenda vyema bila ya kuathiri ratiba nzima iliyowekwa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa misaada inayotowa kwa Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itajitahidi kushirikiana na wahandisi wa Ujenzi huo wa uwanja ili kuona Mradi huo unakamilika katika kipindi kilichokusudiwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaonya Wananchi kuacha tabia ya wizi wa vifaa vilivyotengwa kwa ajili ya kazi hiyo kwani kufanya hivyo ni aibu kwa vile jamii ya Kimataifa itashangaa kuona miradi iliyotengwa kuwanufaisha Wananchi inafanyiwa hujuma.
Aliagiza vyombo vinavyohusika na ulinzi kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu wale wote wanaofanya vitendo viovu vya kutaka kuiba vifaa vya ujenzi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment