Thursday, July 27

Nusu ya watanzania wanasema usalama umeimarika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita; Lakini wananchi wanne kati ya kumi wameshuhudia vurugu zikitokea hadharani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.




27 Julai 2017, Dar es Salaam. Kuna mtazamo wa jumla miongoni mwa wananchi kuwa usalama nchini umeimarika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kama inavyooneshwa na zaidi ya nusu ya wananchi hao (asilimia 53). Lakini asilimia 37 ya watanzania wanasema hali ya usalama imebaki vilevile huku asilimia 10 wanasema hali imekuwa mbaya zaidi.

Takwimu za Sauti za Wananchi za mwaka 2015 zilionesha kwamba asilimia 57 ya wananchi hawakuwahi kuhisi hawako salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi. Lakini mwaka 2017 idadi imeongezeka na kufikia asilimia 71. Kwa ujumla kwa mwaka uliopita, asilimia 29 ya wananchi hawakujisikia salama kutembea kwenye maeneo wanayoishi au waliogopa kufanyiwa uhalifu kwenye nyumba zao (asilimia 26). Asilimia 16 walikiri kukaa majumbani mwao huku wakiwa na hofu ya uhalifu.

Pamoja na viashiria chanya kuhusu usalama, viwango vya uhalifu vinaonekana kuwa juu. Asilimia 41 ya wananchi wamewahi kushuhudia uhalifu ukifanyika hadharani ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Hapa usalama tu: Usalama, polisi na haki nchini Tanzania. Muhtasari huu unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simuza mkononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,805 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) mnamo mwezi Aprili mwaka 2017.

Vilevile takwimu hizi zinaonesha kwamba mara nyingi wananchi hawaombi msaada kwa polisi,hasa pale wanapokuwa wahanga wa uhalifu. Ni mwananchi mmoja tu kati ya wanne (asilimia 26) anayeomba msaada polisi. Hata hivyo, idadi hii inatofautiana kutokana na makundi mbalimbali: matajiri (asilimia 42) na wakazi wa mijini (asilimia 41) wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuomba msaada polisi. Wananchi wengine (asilimia 66), huenda kwanza kwa mwenyekiti wa kijiji/mtaa. Wakati huo huo, idadi kubwa ya wananchi imeripoti kutotoa kabisa taarifa za uhalifu: asilimia 21 wanasema hawatatoa taarifa za uhalifu zilizolenga kaya zao na asilimia 8 wanasema uhalifu kwenye jamii zao hautoripotiwa.

Bila shaka wananchi huamua kutotoa taarifa za uhalifu polisi kutokana na umbali wa vituo. Asilimia 27 ya wananchi hawana kituo cha polisi kwenye kata zao. Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo asilimia 50 wanasema hawana kituo cha polisi kwenye kata zao na asilimia 27 hutumia muda mrefu (zaidi ya dakika 30) kufika kwenye kituo cha polisi.

Pamoja na changamoto za uwepo wa vituo vya polisi, asilimia 47 ya wananchi wanaridhika na huduma zinazotolewa na polisi huku asilimia 26 wakiwa hawaridhiki. Sababu kubwa iliyotolewa ya kuridhika na utendaji wa polisi ni kuwa wanasaidia katika kuzuia uhalifu (asilimia 12 - ya wananchi wote), kutatua uhalifu (asilimia 9) au kwa kuwa wanajali wananchi (asilimia 9). Na sababu kuu ya kutoridhishwa na utendaji wa polisi ni vitendo vya rushwa (asilimia 10),kuchelewa kwao katika kutoa msaada (asilimia 4) na utendaji duni wa kazi (asilimia 2).|

Mbali na wenyeviti wa vijiji/mitaa, wananchi pia wanaweza kupata ulinzi kutoka kwa polisi jamii maarufu kama sungusungu. Asilimia 41 ya wananchi wanasema vikundi hivi vya sungusungu vipo katika maeneo yao. Vikundi hivi ni maarufu zaidi katika maeneo ya vijijini (asilimia 42) kuliko mijini (asilimia 32). Miongoni mwa wenye sungusungu katika maeneo yao, idadi kubwa (asilimia 78) wanaridhika na huduma zinazotolewa na wanasema kuwa hali ya usalama imeimarika kwenye maeneo wanayoishi tangu kuanzishwa kwa sungusungu. 

Wakati imani juu ya hali ya usalama imeongezeka, asilimia 74 ya wananchi wanasema matajiri huadhibiwa mara chache ama hawaadhibiwi kwa mujibu wa sheria wanapofanya uhalifu. Vilevile, wengi wana mashaka juu ya haki kutendeka katika makundi mbalimbali ya watu wenye nguvu katika jamii. 

Angalau wananchi wawili kati ya watatu wanasema watu wafuatao huadhibiwa mara chache ama hawaadhibiwi kabisa: maofisa waandamizi wa serikali (asilimia 72), maofisa wa polisi (asilimia 69), viongozi wa dini (asilimia 68) na watumishi wa umma (asilimia 68). Kundi pekee ambalo wananchi huamini kuwa wanaadhibiwa mara zote kwa mujibu wa sheria ni wananchi wa kawaida (asilimia 65). Hata hivyo, idadi ya wananchi wanaofikiri kuwa mtu yeyote kuanzia mwananchi wa kawaida mpaka tajiri, wana kinga wafanyapo uhalifu imeshuka katika masuala yote tangu mwaka 2015. Mwaka 2017 wananchi walionekana kwa ujumla kuamini kuwa watu wanaweza kuadhibiwa kwa uhalifu waliofanya bila kujali wao ni nani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: ‘Takwimu za muhtasari huu zinatoa taswira tofauti kabisa na ile inayotolewa na vichwa vingi vya habari; kwa mtazamo wa Wananchi wengi, usalama unaonekana kuimarika. Lakini tusijisahau. Imani ya wananchi kwa jeshi la polisi bado ni ndogo. Polisi si kimbilio la kwanza katika utoaji wa taarifa za uhalifu. Polisi wanaweza kufanya jitihada madhubuti za kuwa karibu na wananchi kwa kuanzisha vituo zaidi vya polisi na kujenga imani na uaminifu kwa wananchi.”

No comments:

Post a Comment